Sudan yatishia kulipiza kisasi dhidi ya Kenya kwa kuandaa shughuli za RSF

(CRI Online) Februari 25, 2025

Serikali ya Sudan imesema itachukua hatua kali dhidi ya Kenya kutokana na Kenya kuwa mwenyeji wa shughuli zinazofanywa na wapiganaji wa Vikosi vya Mwitikio wa Haraka (RSF).

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan Bw. Hussein al-Amin amesema kwenye mkutano na wanahabari mjini Port Sudan kuwa, Sudan itawasilisha malalamiko yake kwa Umoja wa Afrika na mashirika mengine ya kimataifa, na ina hatua nyingine zaidi dhidi ya Kenya kutokana na misimamo yake ya kihasama dhidi ya Sudan.

Amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku uagizaji bidhaa za Kenya, hasa kwa vile Sudan ni moja ya waagizaji wakubwa wa chai kutoka Kenya.

Wiki iliyopita makundi ya upinzani ya Sudan, ikiwa ni pamoja na kundi la RSF, walisaini Makubaliano mjini Nairobi, yenye lengo la kuanzisha serikali ya kiraia nchini Sudan.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha