Maafisa wa Ethiopia wapongeza mifumo ya ushirikiano iliyoanzishwa na China kuhimiza maendeleo barani Afrika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 26, 2025

ADDIS ABABA - Maafisa wa Ethiopia wamesema mifumo ya ushirikiano wa maendeleo iliyoanzishwa na China na Afrika inapata matunda kwa kuhimiza maendeleo endelevu, kuimarisha muunganisho wa kikanda na kuhimiza mageuzi ya kiuchumi katika bara zima.

Kwenye Kongamano la Uchumi na Biashara la Ethiopia na China lililofanyika Jumatatu mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, maafisa hao wa Ethiopia wamepongeza ushirikiano kati ya China na Afrika chini ya Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI) na mifumo ya Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).

Negus Kebede, mkurugenzi mkuu wa masuala ya Mashariki ya Kati, Asia na Pasifiki katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia, amesema FOCAC imekuwa ikihimiza maendeleo endelevu, amani na usalama kote barani Afrika.

Akibainisha kuwa China ni mwekezaji mkuu katika sekta ya viwanda ya Ethiopia, ikiwa na miradi zaidi ya 3,000 inayozalisha ajira karibu 600,000 kwa Waethiopia, Kebede amesema Reli ya Ethiopia-Djibouti, mradi kinara chini ya BRI, unachochea ushirikiano wa kikanda barani Afrika.

"Sisi Waafrika tunathamini uungaji mkono wa China katika kupunguza mzigo wa madeni wa nchi zao kupitia njia za pande nyingi na za pande mbili, vilevile mchango wake katika kuhimiza mawasiliano ya kielimu, kiutamaduni na kiteknolojia kupitia ufadhili wa masomo, mafunzo ya ufundi na ubia wa utafiti," amesema.

Amebainisha kuwa Kituo cha Ubora cha China-Afrika-UNIDO mjini Addis Ababa ni mpango mwingine wa kupongezwa, ukitumika kama jukwaa la kuhimiza maendeleo endelevu ya viwanda, kuendeleza mambo ya kisasa kwenye kilimo, na kuimarisha maendeleo ya ujuzi kote Afrika.

Akibainisha kuwa China ilitangaza sera ya kutotoza ushuru bidhaa kutoka nchi zilizoko nyuma kimaendeleo ambazo zina uhusiano wa kidiplomasia na China, Waziri wa Biashara na Ushirikiano wa Kikanda wa Ethiopia Yasmin Wohabrebbi amesema nchi nyingi za Afrika zinanufaika na sera hiyo na kuuza bidhaa zao katika soko la China.

Waziri huyo pia amepongeza dhamira ya China katika kupanua biashara ya mtandaoni na ushirikiano wa kidijitali na Afrika.

Takwimu kutoka wizara hiyo zinaonyesha kuwa bidhaa kuu za Ethiopia zinazouzwa China ni pamoja na kahawa, mbegu za mafuta, ngozi na bidhaa za ngozi, pamba na uzi. Wakati huo huo, Ethiopia inaagiza bidhaa mbalimbali kutoka China, zikiwemo magari, vitambaa na nguo, mashine na viatu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha