

Lugha Nyingine
Ripoti yaonesha China inaendelea kuwa eneo linalovutia la uwekezaji
Picha hii ikionyesha Eneo Maalum la Viwanda vya Petroli na Kemikali la Ghuba ya Daya ya Huizhou ambako Miradi ya Ethylene wa Awamu ya Tatu na ule wa Polycarbonate inapatikana, Mkoani Guangdong, kusini mwa China. (Xinhua)
GUANGZHOU – Shirikisho la Wafanyabiashara wa Marekani Kusini mwa China (AmCham South China) jana Jumatano limetoa ripoti yake maalum ya mwaka 2025 juu ya Hali ya Biashara Kusini mwa China, ambayo inaonyesha kuwa nchi hiyo yenye uchumi wa pili kwa ukubwa duniani inaendelea kuwa eneo linalovutia la uwekezaji.
Ripoti hiyo ya mwaka huu, ambayo ni ya 21 katika mfululizo wake, inatoa uchambuzi wa kina na wa kitakwimu wa jumuiya ya wafanyabiashara, ikitoa mambo muhimu kuhusu mwelekeo wa maendeleo katika eneo la Kusini mwa China. Kampuni jumla ya 316 zimeshiriki katika utafiti huo wa mwaka 2024.
Ripoti hiyo inaangazia nafasi ongozi ya China katika vipaumbele vya uwekezaji duniani, huku asilimia 58 ya kampuni hizo za kigeni zilizohojiwa zikiiweka miongoni mwa vipaumbele vyao vitatu vya juu vya uwekezaji.
Ikiangalia siku zijazo katika mwaka 2025, ripoti hiyo inaonesha kuwa, asilimia 76 ya kampuni hizo zinakusudia kuwekeza tena nchini China, huku asilimia 74 ya kampuni za Marekani zikipanga kufanya uwezekezaji tena, ikiwa ni ongezeko la asilimia 11 kuliko mwaka uliotangulia.
Kampuni hizo zilizofanyiwa hojaji ni hasa kutoka Marekani, China, na Umoja wa Ulaya. Ripoti hiyo inaonesha kuwa, zaidi ya nusu ya kampuni hizo zinamilikiwa na wageni kabisa, na zaidi ya asilimia 30 zimewekezwa kwa mtaji wa Marekani.
Aidha ripoti hiyo inasema kuwa, idadi ya kampuni zilizozalisha asilimia zaidi ya 60 ya mapato yao ya kimataifa kutoka China zimeongezeka kwa asilimia 5, zikifikia jumla ya asilimia 31.
"Uwezo wa ukuaji wa soko la China unaendelea kuwa kichocheo kikuu cha kuongeza uwekezaji nchini China au kuhamisha uwekezaji kutoka masoko mengine hadi China, ikifuatiwa na mchango wa makundi ya viwanda na sera za upendeleo," amesema Harley Seyedin, Mwenyekiti na Rais wa AmCham South China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma