

Lugha Nyingine
Watu 11 wauawa na wengine 65 kujeruhiwa katika milipuko baada ya mkutano mashariki mwa DRC
Picha ya skrini kutoka kwenye video ikionyesha watu wakihamisha mtu aliyejeruhiwa katika mlipuko mjini Bukavu, Jimbo la Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Februari 27, 2025. (Xinhua)
KINSHASA - Milipuko kadhaa imesababisha vifo vya watu wapatao 11 na wengine 65 kujeruhiwa jana Alhamisi mjini Bukavu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), muda mfupi baada ya mkutano wa kisiasa wa kuunga mkono kundi la waasi la M23 ambapo tukio jipya la vifo na majeruhi limethibitishwa na Corneille Nangaa, kiongozi wa kisiasa wa Muungano wa Mto Kongo, kundi la kisiasa na kijeshi lenye ushirikiano na M23.
Milipuko hiyo imetokea muda mfupi baada ya mkutano huo, ambao Nangaa alikuwa akiuhutubia kwenye uwanja wa Uhuru katika mji mkuu huo wa Jimbo la Kivu Kusini.
M23 imeitupia lawama serikali ya DRC kwa milipuko hiyo, ikisema kuwa baadhi ya washambuliaji wamejeruhiwa au kuuawa, na kwamba washukiwa wawili wamekamatwa. Nangaa amesema kuwa yeye na viongozi wengine waandamizi wa kundi hilo la waasi waliokuwepo kwenye mkutano huo hawakujeruhiwa.
Rais wa DRC Felix Tshisekedi amelaani mashambulizi hayo katika taarifa yake, akitoa salamu zake za rambirambi kwa familia zilizopoteza watu hao waliouawa.
"Hatutajiondoa. Tuko nyumbani," Nangaa alisema mapema kwenye mkutano huo wa kisiasa, akiahidi kuteua gavana wa Jimbo la Kivu Kusini na meya wa Bukavu.
Pia ameahidi kukarabati barabara kati ya Bukavu na Goma, mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini. M23 imedai kudhibiti miji yote hiyo miwili. Mapema mwezi huu, kundi hilo la waasi lilianzisha utawala sambamba jimboni Kivu Kaskazini.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Operesheni za Amani Jean-Pierre Lacroix ameonya kwamba mgogoro huo wa DRC unaweza kuzidi kuongezeka kuwa mgogoro mkubwa zaidi wa kikanda. "Uwezekano wa kuenea kikanda kutokana na mgogoro huo wa DRC ni uhalisia," Lacroix ameandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X, zamani Twitter.
"Kuongezeka hali ya wasiwasi ya kikanda lazima kuepukwe kwa gharama yoyote," Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema hivi karibuni katika Mkutano wa 38 wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia. "Hakuna suluhu ya kijeshi. Mkwamo lazima ukome, na mazungumzo lazima yaanze."
Picha ya skrini kutoka kwenye video ikionyesha watu wakihamisha mtu aliyejeruhiwa katika mlipuko mjini Bukavu, Jimbo la Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Februari 27, 2025. (Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma