

Lugha Nyingine
Sierra Leone yazindua kituo cha kwanza cha dawa za jadi za Kichina
![]() |
Wawakilishi wa China na Sierra Leone wakihudhuria hafla ya uzinduzi wa kituo cha kwanza cha dawa za jadi za Kichina (TCM) mjini Freetown, Sierra Leone, Februari 28, 2025. (Kundi la 25 la Timu ya Madaktari wa China nchini Sierra Leone/kupitia Xinhua) |
FREETOWN - Kituo cha kwanza cha dawa za jadi za Kichina (TCM) nchini Sierra Leone kimezinduliwa Ijumaa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Freetown, ikiashiria hatua muhimu katika juhudi za nchi hiyo kuanzisha tiba ya TCM kwa manufaa ya watu wake.
Kuzinduliwa kwa kituo hicho cha TCM kumekuja baada ya kukamilika kwa mradi wa uchunguzi wa afya ya jamii nchini Sierra Leone, ulioongozwa na kundi la madaktari wa China, ambao ulilenga kusaidia nchi hiyo ya Afrika Magharibi kuboresha kinga na matibabu dhidi ya magonjwa ya kawaida kama vile shinikizo la damu na maumivu sugu.
You Xiong, naibu mkuu wa kundi la 25 la timu ya madaktari wa China nchini Sierra Leone, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kuwa wakati wa mradi huo, huduma za bila malipo za matibabu ya acupuncture zilitolewa kwa maelfu ya wanajamii kote nchini humo.
"Mradi wetu ulionyesha ufanisi wa uwezo wa acupuncture katika kusimamia shinikizo la damu na maumivu sugu, ukipokea maoni mazuri kutoka kwa wagonjwa wenyeji," amesema You, ambaye aliongoza mradi huo.
Akihutubia hafla ya uzinduzi wa kituo hicho, Charles Senessie, naibu waziri wa afya wa Sierra Leone, amepongeza ushirikiano wa kudumu kati ya Sierra Leone na China katika sekta ya afya, hasa katika kuendeleza matumizi ya tiba za jadi. Amesema kuwa Sierra Leone imepiga hatua kubwa katika kujumuisha TCM katika mfumo wake wa afya wa kitaifa.
Naibu waziri huyo pia ameelezea matumaini kuwa kituo hicho kipya cha TCM kitatoa mafunzo kwa madaktari wenyeji zaidi katika TCM, na kuwawezesha kutoa huduma bora za matibabu kwa wakazi wa vijijini.
China ilituma timu yake ya kwanza ya madaktari nchini Sierra Leone mwaka 1973 na tangu wakati huo imeshatuma timu 25, zikitoa mchango mkubwa katika sekta ya afya ya nchi hiyo na kukuza uhusiano wa jadi wa urafiki.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma