Kilimo cha juu ya paa la nyumba chageuza kijiji cha Misri kilichokuwa maskini kuwa ardhi inayostawi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 03, 2025

Mkulima akitunza bustani ya mboga juu ya paa la nyumba katika Kijiji cha Nagaa Aoun, Mkoa wa Beheira, Misri, Februari 18, 2025. (Xinhua/Ahmed Gomaa)

Mkulima akitunza bustani ya mboga juu ya paa la nyumba katika Kijiji cha Nagaa Aoun, Mkoa wa Beheira, Misri, Februari 18, 2025. (Xinhua/Ahmed Gomaa)

BEHEIRA – Nagaa Aoun, kijiji katika Mkoa wa Beheira nchini Misri, kilikuwa katika hali ya dhiki, lakini sasa kimepitia mageuzi makubwa. Kupitia kilimo bunifu cha juu ya mapaa ya nyumba, kijiji hicho kimejitosheleza kwa mboga za majani na kufurahia mapato ya kutosha.

Mwongoza juhudi hizo ni Ragab Rabie, jamaa mwenye umri wa miaka 45 ambaye alianzisha dhana hiyo katika kijiji hicho miaka 10 iliyopita.

Rabie ambaye aliwahi kuwa mvuvi, alihamasishwa na video ya mkulima wa China akipanda mazao juu ya paa la nyumba yake. Akiiona kama fursa ya kuboresha vyote hali yake ya kifedha na ya wanakijiji wenzake, alianza kutafuta njia za kutekeleza wazo hilo kijijini.

Kijiji hicho, kilicho kati ya maziwa madogo ya chumvi na ardhi isiyo na tija, hapo awali kilikuwa kikikabiliwa na matatizo ya kiuchumi. Jamaa wengi walifanya kazi za vibarua za kutwa katika miji ya karibu, wakitafuta kazi za ujenzi, ukarabati wa magari, na kilimo.

Baada ya kutafiti kilimo cha maji kisichotumia udongo (hydroponic farming), Rabie alishawishi wakazi kadhaa kushiriki katika mradi wa majaribio.

"Changamoto ya awali ilikuwa kwamba nyumba nyingi katika kijiji hicho zilijengwa kwa kuezekwa kwa majani na matete, ambayo hayafai kwa kilimo cha juu ya paa. Hata hivyo, kwa msaada wa mikopo kutoka kwa benki na taasisi za mikopo, wanakijiji wengi waliweza kujenga nyumba mpya zenye mapaa ya saruji, ambayo ni mwafaka zaidi kwa kufunga vitengo vya hydroponiki," Rabie ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.

Wakulima wawili wakitunza bustani ya mboga juu ya paa la nyumba katika kijiji cha Nagaa Aoun, Mkoa wa Beheira, Misri, Februari 18, 2025. (Xinhua/Ahmed Gomaa)

Wakulima wawili wakitunza bustani ya mboga juu ya paa la nyumba katika kijiji cha Nagaa Aoun, Mkoa wa Beheira, Misri, Februari 18, 2025. (Xinhua/Ahmed Gomaa)

Leo, wanakijiji wa Nagaa Aoun wanavuna manufaa ya kilimo hicho cha juu ya mapaa. Rabie amesema kuwa kila kitengo cha hydroponic, chenye upana wa sentimita 105 na urefu wa mita 3, kinaweza kutoa miche 405, sawa na pato la ardhi ya mita za mraba 175.

Vitengo hivyo vinaweza kulimwa mara nne kwa mwaka, kwa kutumia chini ya robo ya maji yanayohitajika kwa mbinu za kawaida za kilimo, kwani mfumo huo wa hydroponic husambaza maji kwa njia maalum inayofungwa na hivyo kupunguza upotevu wa maji.

Kwa mujibu wa Rabie, mradi huo umepunguza kwa kiasi kikubwa ukosefu wa ajira katika kijiji hicho kwa asilimia 95 na kuboresha hali ya maisha, na wakazi wananufaika na makazi, mavazi na chakula bora.

Rabie anaamini kuwa suluhu bunifu kama vile kilimo hicho cha juu ya paa ni muhimu kwa mustakabali wa kilimo cha Misri, kwa kuwa ni asilimia 3-4 tu ya ardhi ya nchi hiyo ndiyo inayoweza kulimwa.

"Wanakijiji hawamiliki ardhi ya kilimo, lakini wanamiliki mapaa ya nyumba zao," amesema.

Rabie pia amekuwa akifuatilia maendeleo ya teknolojia ya kilimo hicho cha juu ya mapaa cha China na anatarajia kushirikiana na kampuni za China kuboresha uzalishaji na mapato ya wenyeji.

"China imepiga hatua katika nyanja ya kilimo cha juu ya mapaa, na tunaweza kujifunza mengi kutokana na uzoefu na teknolojia yao," amesema Rabie.

Mkulima akitunza bustani ya mboga juu ya paa la nyumba katika kijiji cha Nagaa Aoun, Mkoa wa Beheira, Misri, Februari 18, 2025. (Xinhua/Ahmed Gomaa)

Mkulima akitunza bustani ya mboga juu ya paa la nyumba katika kijiji cha Nagaa Aoun, Mkoa wa Beheira, Misri, Februari 18, 2025. (Xinhua/Ahmed Gomaa)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha