Pembe ya Afrika yatarajiwa kuwa na joto kuliko kawaida kuanzia Machi hadi Mei

(CRI Online) Machi 04, 2025

Kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa (ICPAC) cha Mamlaka ya Maendeleo ya Kiserikali ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) kimeripoti kwamba pembe ya Afrika inatarajiwa kuwa na joto zaidi kuliko kawaida kuanzia Machi hadi Mei, isipokuwa kusini mashariki mwa Sudan Kusini na kaskazini mashariki mwa Uganda.

Kituo hicho kimeeleza, hali ya joto katika kipindi hiki inaweza kuzidi nyuzi joto 32 za Celsius katika baadhi ya nchi, huku maeneo kadhaa yakiwemo magharibi na kusini magharibi mwa Kenya, mashariki mwa Uganda, mashariki mwa Sudan Kusini, magharibi mwa Ethiopia na maeneo mengi ya Tanzania, yakitarajiwa kukumbwa na hali ya mvua kuliko kawaida.

Kimefafanua kuwa, hali ya ukame kuliko kawaida imetabiriwa katika sehemu nyingi za Ethiopia, Somalia, Djibouti, Kenya, Rwanda, Burundi, sehemu ya magharibi ya Uganda na Sudan Kusini.

Imeelezwa kuwa, matatizo hayo ya hali ya hewa yanasababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na IGAD, watu wapatao milioni 66.9 katika eneo hilo wanakabiliwa na uhaba wa chakula, idadi ambayo huenda ikaongezeka kutokana na kuongezeka kwa hali ya hewa isiyo ya kawaida.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha