Trump atoa msamaha wa mwezi mmoja kwa kampuni tatu za magari kutoka ushuru wa Mexico na Canada

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 06, 2025

Msemaji wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kwenye Ikulu ya White House mjini Washington, D.C., Marekani, Machi 5, 2025. (Xinhua/Hu Yousong)

Msemaji wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kwenye Ikulu ya White House mjini Washington, D.C., Marekani, Machi 5, 2025. (Xinhua/Hu Yousong)

WASHINGTON - Ikulu ya White House imesema kwamba Rais wa Marekani Donald Trump ametoa msamaha wa mwezi mmoja kwa kampuni tatu kuu za magari kutoka kwenye ushuru mpya wa asilimia 25 uliowekwa kwa Mexico na Canada.

"Tulizungumza na wafanyabiashara watatu wakubwa wa magari (watengenezaji), tutakwenda kutoa msamaha wa mwezi mmoja kwa magari yoyote yanayokuja kupitia USMCA. Ushuru wa kutozana kwa usawa bado utaanza kutumika Aprili 2," Msemaji wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt amewaambia waandishi wa habari katika mkutano na waandishi wa habari jana Jumatano.

Levitt amesema Trump amezungumza na kampuni tatu -- Ford, General Motors, na Stellantis -- na zimetoa ombi hilo ambapo rais amekubali kuwapa msamaha huo wa ushuru kwa mwezi mmoja.

Chombo cha habari cha Bloomberg kiliripoti mapema Jumatano kwamba Trump atakuwa akizipa msamaha kampuni hizo za kuunda magari kutoka kwenye ushuru mpya uliowekwa kwa Mexico na Canada kwa mwezi mmoja, "kama ahueni ya muda kufuatia maombi ya viongozi wa tasnia."

Makubaliano ya Marekani-Mexico-Canada (USMCA) ni makubaliano ya kibiashara yaliyojadiliwa, kutiwa saini, na hatimaye kupitishwa wakati wa muhula wa kwanza wa Trump, yenye lengo la kuwa mbadala wa Mkataba wa Biashara Huria wa Amerika Kaskazini (NAFTA).

Chini ya USMCA, ununuzi wa vipuri vya magari lazima utimize sheria mahsusi ili kuwa na sifa za kupita chini ya ushuru huria.

Februari 1, Trump alitia saini amri tendaji ya kutoza ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa zinazoagizwa nje kutoka Mexico na Canada, huku kukiwa na ongezeko la ushuru la asilimia 10 kwa bidhaa za nishati za Canada. Februari 3, Trump alitangaza ucheleweshaji wa siku 30 katika kutekeleza ushuru huo kwa nchi zote mbili na kuendeleza majadiliano. Kwa mujibu wa uamuzi huo, hatua husika za ushuru zimeanza kutumika Machi 4.

Rais wa Marekani Donald Trump akihudhuria mkutano na waandishi wa habari kwenye Ikulu ya White House mjini Washington, D.C., Marekani, Februari 14, 2025. (Xinhua/Hu Yousong)

Rais wa Marekani Donald Trump akihudhuria mkutano na waandishi wa habari kwenye Ikulu ya White House mjini Washington, D.C., Marekani, Februari 14, 2025. (Xinhua/Hu Yousong)

Trump Jumanne usiku alitetea mkakati wake huo wa ushuru wakati akitoa hotuba kwenye kikao cha pamoja cha Bunge la Seneti na lile la Congress, lakini alikiri kwamba sera kama hizo zitasababisha "mvurugano kidogo."

Hata hivyo, wachumi na waangalizi wa mambo wameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu athari tarajiwa za ushuru huo kwa uchumi wa Marekani.

Taasisi ya Ushuru imekadiria kuwa, bila kuzingatia hatua za kulipiza, ushuru huo wa asilimia 25 wa Trump kwa Canada na Mexico, ambao ulianza kutumika Jumanne wiki hii, utapunguza Pato la Taifa la muda mrefu kwa asilimia 0.2, kupunguza saa za kufanya kazi kwa sawa na ajira kamili 223,000, na kupunguza mapato ya baada ya ushuru kwa wastani wa asilimia 0.6.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha