Namibia yatoa noti za ukumbusho kwa heshima ya marehemu Rais Geingob

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 06, 2025

Gavana wa Benki ya Namibia Johannes Gawaxab akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa noti ya ukumbusho ya Hage Geingob mjini Windhoek, Namibia, Machi 5, 2025. (Picha na Musa C Kaseke/Xinhua)

Gavana wa Benki ya Namibia Johannes Gawaxab akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa noti ya ukumbusho ya Hage Geingob mjini Windhoek, Namibia, Machi 5, 2025. (Picha na Musa C Kaseke/Xinhua)

WINDHOEK - Rais wa Namibia Nangolo Mbumba amezindua noti ya ukumbusho ya Hage Geingob Jumatano katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika mjini Windhoek, mji mkuu wa nchi hiyo ambapo noti hiyo imezinduliwa kwa heshima ya michango ya kipekee ya marehemu rais wa zamani wa nchi hiyo Hage Geingob ambaye aliaga dunia Februari 4, 2024, alipokuwa akipokea matibabu ya saratani.

Rais Mbumba, katika hotuba yake kuu, amempongeza marehemu rais huyo, akibainisha kuwa alikuwa "mjenzi wa taifa."

“Noti hiyo inaimarisha maono na michango yake kwa Namibia, huku noti hiyo maalum ikitumika kama kumbukumbu ya kudumu kwa mchango wake kwa taifa,” amesema.

Noti hiyo ya thamani ya dola 60 za Namibia, ambayo ina umaalum wa kipekee na chapa ya mara moja, itatumika kama zabuni halali.

Gavana wa Benki Kuu ya Namibia Johannes Gawaxab ameelezea kwamba Geingob alitumia miaka 60 ya maisha yake kwa huduma ya kujitolea kwa taifa hilo, ikijumuisha muda wake wa kuishi uhamishoni, kurejea kwake nchini, na uongozi wake katika Namibia huru.

"Kwa hivyo, namba 60 ina maana kubwa ya kiishara, ikionyesha dhamira yake ya muda mrefu kwa nchi katika miongo hii yote," ameongeza.

Gawaxab pia amesema benki hiyo kuu itaanzisha mfululizo mpya wa noti na sarafu mwezi Juni. "Mfululizo huu utajumuisha vipengele vya hivi punde zaidi vya kiusalama huku tukihakikisha noti na sarafu zetu zinaendelea kuwa za kisasa, thabiti na salama."

Mwaka 2020, katika kusherehekea miaka 30 tangu uhuru wa Namibia, Benki Kuu ya Namibia ilitoa noti yake ya kumbukumbu ya kwanza kabisa, noti yenye thamani ya dola 30 za Namibia, iliyochapishwa kwenye kipande cha polima kwa uimara zaidi.

Noti hiyo ina nyuso za Rais mwasisi wa Namibia Sam Nujoma, Rais wa zamani Hifikepunye Pohamba na Geingob, ikiashiria ukabidhianaji kwa amani madaraka na urithi wa amani, utulivu na maendeleo.

Picha iliyopigwa Machi 5, 2025 ikionyesha noti ya ukumbusho ya Hage Geingob kwenye hafla ya uzinduzi wake mjini Windhoek, Namibia. (Picha na Musa C Kaseke/Xinhua)

Picha iliyopigwa Machi 5, 2025 ikionyesha noti ya ukumbusho ya Hage Geingob kwenye hafla ya uzinduzi wake mjini Windhoek, Namibia. (Picha na Musa C Kaseke/Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha