

Lugha Nyingine
Wanafunzi 32 wa Zimbabwe kusomea mekatroniki nchini China chini ya mpango wa mafunzo ya pamoja
Wanafunzi wakiwa katika picha ya pamoja na maofisa wa serikali za Zimbabwe na China kwenye hafla ya kuwaaga katika Chuo cha Ufundi cha Harare mjini Harare, Zimbabwe, Machi 6, 2025. (Picha na Shaun Jusa/Xinhua)
HARARE - Wanafunzi 32 wa Zimbabwe kutoka Chuo cha Ufundi cha Harare watakwenda China kusomea uhandisi wa mekatroniki kwa muda wa miezi 18 katika Chuo cha Ufundi cha Ningbo, Mkoa wa Zhejiang, mashariki mwa China chini ya mpango wa mafunzo ya pamoja kati ya vyuo hivyo viwili vya ufundi.
Chini ya mpango huo, wanafunzi hao tayari wamemaliza mwaka wao wa kwanza wa masomo nchini Zimbabwe.
Akizungumza kwenye hafla ya kuwaaga wanafunzi hao iliyofanyika katika Chuo hicho cha Ufundi cha Harare siku ya Alhamisi katika mji mkuu, Harare, Naibu Waziri wa Elimu ya Juu na Ufundi, Maendeleo ya Uvumbuzi, Sayansi na Teknolojia wa Zimbabwe Simelisizwe Sibanda amesema mpango huo unaashiria hatua muhimu katika juhudi za ushirikiano wa kimataifa wa elimu wa Zimbabwe.
"Ushirika wa muda mrefu kati ya Zimbabwe na China unaokita mizizi katika uhusiano wa kihistoria umepitia hali mbalimbali na kuwa ushirikiano wenye ustawi katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu," Sibanda amesema.
Amesema, hadi kufikia sasa, wanafunzi 58 kutoka makundi mawili wameshaingia kwenye mpango huo unaofadhiliwa kikamilifu, ambao hutoa vyeti viwili kutoka vyuo vyote viwili vya ufundi vya Harare na Ningbo.
Ushirikiano huo tayari umepata matokeo chanya, Sibanda amesema, akiongeza kuwa wanafunzi 30 waliosafiri kwenda China chini ya mpango huo mwaka 2023 wameshamaliza mafunzo yao na tayari wamepata ajira.
"Hii inaonyesha ufanisi wa programu hii katika kuziba pengo muhimu la ujuzi na kuhakikisha kuwa wahitimu wanachangia ipasavyo katika ajenda ya maendeleo ya viwanda ya Zimbabwe," amesema Sibanda.
Panashe Mudondo, mmoja wa wanufaika wa mpango huo, amesema utawajenga wanafunzi kwa ujuzi hitajika ili kuhimiza maendeleo ya taifa.
"Tunashukuru kwa maono na dhamira ya serikali yetu kuwekeza katika elimu na maendeleo yetu. Fursa hii inakwenda kufanya njia yetu ya kazi kuwa maalum. Ninatumai na kuamini kwamba tutarejesha mawazo mapya kwa njia tofauti na kuwa sehemu muhimu ya ajenda ya maendeleo ya viwanda na ujenzi wa mambo ya kisasa wa Zimbabwe," amesema.
Afisa wa serikali ya Zimbabwe akizungumza na wanafunzi kwenye hafla ya kuwaaga katika Chuo cha Ufundi cha Harare mjini Harare, Zimbabwe, Machi 6, 2025. (Picha na Shaun Jusa/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma