Ethiopia yawarejesha nyumbani raia 287 waliokuwa wamezuiliwa nchini Kenya

(CRI Online) Machi 07, 2025

Serikali ya Ethiopia imetangaza kuwarejesha nyumbani raia 287 waliokuwa wamezuiliwa katika magereza 18 sehemu mbalimbali nchini Kenya.

Ubalozi wa Ethiopia nchini Kenya umesema katika taarifa yake Jumatano kwamba watu hao walikuwa wazuiliwa na mamlaka ya Kenya baada ya kuingia nchini humo kinyume cha sheria walipokuwa wakijaribu kwenda Afrika Kusini, baada ya kuvutwa na walanguzi wa binadamu.

Kufuatia uratibu wa karibu kati ya ubalozi na serikali ya Kenya, raia hao wa Ethiopia walirejea nyumbani Jumatano kupitia usafiri wa ardhini wakivuka mpaka wa Moyale.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, maelfu ya Waethiopia husafiri katika njia ya uhamiaji ya kusini kila mwaka, wakitarajia kufika Afrika Kusini. Wengi wao hudanganywa na walanguzi ambapo husafiri kupitia Kenya, Tanzania, na nchi nyingine za kusini mwa Afrika, huku wakikabiliwa na vifungo na matatizo mengi njiani.

Mbali na kuwekwa kizuizini, wahamiaji hao waliokata tamaa mara nyingi hukumbwa na hatari zinazotishia maisha yao njiani.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha