

Lugha Nyingine
Rais wa Ghana aahidi kurejesha kuaminiana kati ya jumuiya za kikanda
Rais wa Ghana John Dramani Mahama (kushoto) akikutana na Rais wa Mali Assimi Goita mjini Bamako, Mali, Machi 8, 2025. (Picha na Habib Kouyate/Xinhua)
BAMAKO - Rais wa Ghana John Dramani Mahama siku ya Jumamosi amesisitiza dhamira yake ya kurejesha kuaminiana kati ya Muungano wa Nchi za Sahel na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS).
Akizungumzia hali ya kutoelewana inayoendelea kati ya muungano huo na ECOWAS, Mahama amekiri "kuvunjika kwa kuaminiana" na kuhakikisha kwamba "tutafanya kila liwezekanalo kurejesha kuaminiana huku."
Mahama ametoa kauli hiyo kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Bamako wakati wa ziara yake nchini Mali, na amesisitiza kuwa ziara yake hiyo kimsingi inalenga kuimarisha uhusiano wa pande mbili.
"Majadiliano yetu yalijikita katika uhusiano wa pande mbili, hasa mabadilishano ya kiuchumi, na mchango wa wanadiaspora wa Mali nchini Ghana kwa uchumi wa nchi zote mbili," amewaambia waandishi wa habari.
Viongozi hao wawili pia walijadili kufufua kamisheni ya ushirikiano wa pamoja na masuala ya usalama, hasa mapambano dhidi ya ugaidi.
Januari 28, 2024, Burkina Faso, Mali na Niger kwa pamoja zilitangaza nia ya kujitoa ECOWAS kufuatia vikwazo vya awali vilivyowekwa na jumuiya hiyo ya kikanda ili kushinikiza viongozi wa kijeshi katika nchi hizo na kurejea nchi hizo kwenye utaratibu wa kikatiba.
Nchi hizo tatu zilizojitenga zilitangaza kuundwa kwa Shirikisho la Muungano wa Nchi za Sahel kwenye mkutano wa kwanza wa viongozi wa shirikisho hilo nchini Nigeria, Julai 6, 2024.
Kuanzia Januari 29, Burkina Faso, Mali na Niger si nchi wanachama tena wa ECOWAS lakini zimepewa muda wa ziada wa kufikiria upya uamuzi wao huo. Wakati huo huo, Ghana imekuwa ikiimarisha uhusiano wake na muungano huo wa Nchi za Sahel na kueleza utayari wake wa kuwezesha kujumuishwa tena kwa mataifa hayo matatu katika ECOWAS.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma