Kampuni ya China kuongoza mradi wa kurejesha ikolojia ya Mto Nairobi nchini Kenya

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 11, 2025

Rais wa Kenya William Ruto (wa pili, kulia) akihudhuria hafla ya uwekaji jiwe la msingi la mradi wa kurejesha ikolojia ya Mto Nairobi jijini Nairobi, Kenya, Machi 10, 2025. (Xinhua/Han Xu)

Rais wa Kenya William Ruto (wa pili, kulia) akihudhuria hafla ya uwekaji jiwe la msingi la mradi wa kurejesha ikolojia ya Mto Nairobi jijini Nairobi, Kenya, Machi 10, 2025. (Xinhua/Han Xu)

NAIROBI - Rais wa Kenya William Ruto Jumatatu aliongoza hafla ya uwekaji jiwe la msingi kwa ajili ya mradi wa ulinzi na urejeshaji wa Bonde la Mto Nairobi, mradi utakaotekelezwa na Kampuni ya Energy China.

Maafisa waandamizi wa serikali, watendaji kutoka kampuni ya Energy China, na watetezi wa mazingira pia walihudhuria hafla hiyo, ambayo inalenga kurejesha ustawi wa kiikolojia wa Mto Nairobi unapopitia mji mkuu.

Uboreshaji wa Bonde la Mto Nairobi utaendeshwa na mradi wa nyumba za bei nafuu, ukiwa umepangwa kutekelezwa kwa muda wa miaka minne kwa gharama ya shilingi bilioni 50 za Kenya (dola za Kimarekani karibu milioni 388).

Ruto amesema kurejesha hadhi ya kiikolojia ya Mto Nairobi baada ya miongo kadhaa ya uchafuzi wa mazingira kutatengeneza ajira mpya kwa vijana, kuboresha afya ya umma, na kuimarisha uendelevu wa mazingira ya mji huo mkuu.

"Mradi huu utatupatia fursa ya kupanua na kuongeza kina cha Mto Nairobi huku tukijenga njia ya maji taka ya urefu wa kilomita 60 kubeba maji machafu, ikiifanya Nairobi kuwa jiji safi na linaloheshimika zaidi," Ruto amesema.

Ameongeza kuwa, ujenzi huo wa nyumba zenye hadhi, zilizounganishwa na mfumo wa kisasa wa maji taka kando ya Bonde la Mto Nairobi lililokarabatiwa, utawezesha uhamishaji wa waathirika wa mafuriko.

Mto Nairobi unatoka katika mitaa ya kaskazini-magharibi mwa mji mkuu wa Kenya, ukitiririka kupitia maeneo ya makazi ya kusini mashariki, lakini kwa muda mrefu umekuwa ukikumbwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira na mafuriko wakati wa msimu wa mvua.

Mwezi Februari mwaka huu, serikali ya Kenya ilitia saini mkataba na Kampuni ya Uhandisi ya Energy China ili kutekeleza awamu ya kwanza ya mradi huo.

Ukiwa umefadhiliwa na serikali ya Kenya, mradi huo unajumuisha ujenzi wa mabomba makuu ya maji taka na mitambo ya kutibu maji machafu, ulinzi wa vyanzo vya maji vya juu ya mito, uchimbuaji wa mto, udhibiti wa maji ya mvua, ushughulikiaji wa taka ngumu, utengenezaji mandhari, na ujenzi wa nyumba za bei nafuu.

Baada ya kukamilika, mradi huo unatarajiwa kupunguza mafuriko kando ya Bonde la Mto Nairobi, kuboresha hali ya maisha ya wenyeji na kubadilisha mandhari ya mjini.

Kwa mujibu wa Li Cheng, meneja wa mradi anayefanya kazi kampuni ya Energy China, ukarabati wa Mto Nairobi unatarajiwa kuchukua miaka miwili, huku jamii za pembezoni zikitarajiwa kufaidika kutokana na uboreshaji mkubwa wa mazingira utakapokamilika.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha