

Lugha Nyingine
Treni ya mwendo wa polepole yaharakisha ustawishaji vijijini China
Abiria wakipanda na kushuka treni Na. 6064 kwenye Stesheni ya Reli ya Yangpingguan mjini Hanzhong, Mkoa wa Shaanxi, kaskazini-magharibi mwa China, Februari 17, 2025. (Xinhua/Shao Rui)
XI'AN, March - Mapambazuko yanapoanzisha siku mpya juu ya milima katika Mkoa wa Shaanxi kaskazini-magharibi mwa China, treni nambari 6064 huunguruma kuleta uhai, ikikata kasi kuupita ukungu na kuamsha mabonde yenye usingizi.
Ikiwa na urefu wa kilomita 350 kutoka Guangyuan, Mkoa wa Sichuan kusini-magharibi mwa China hadi Baoji katika mkoa wa jirani wa Shaanxi, treni inayofanya usafiri wa saa 11 kila mara inapita stesheni 33, na nauli ya tiketi inaanzia yuan 4 tu (kama senti 56 za Marekani).
Mabehewa ya treni yanayotumika kama soko la wakulima na maktaba yao, treni hiyo ya mwendo wa polepole ya nauli chini inawapa urahisi abiria wa vijijini kuuza mazao yao kwa gharama chini, kuwasaidia kupata elimu, na kufanya mawasiliano na nje ya nyumbani kwao.
Jiang Minglin mwenye umri wa karibia miaka 70, amekuwa akitegemea treni hiyo katika miongo kadhaa iliyopita, akibeba mboga freshi za majani ya kilo 30 kila baada ya siku mbili kuuza katika miji ya wilaya jirani.
Jiang amesema kuwa kutokana na wanawe kukua na kupata kazi ya kuaminika, kuuza mazao ya shambani siyo tena kwa kuchuma pesa tu. " Sipendi kukaa bila kufanya kazi. Ninafurahia kufanya kazi na inanifanya kuushughulisha mwili."
Behewa moja kwenye treni hiyo limetengwa mahsusi kwa ajili ya wakulima kama Jiang, likiwa na rafu maalum za vikapu vya mboga za majani na vizimba vya kuku, pamoja na ubao wa taarifa unaoonyesha bei za bidhaa mbalimbali za kilimo. Behewa lingine linatumika kama "maktaba," likitoa vitabu 3,300 kwa wanafunzi.
Mwaka 2023, huduma za matibabu zilianza kutolewa kwenye treni hiyo ya kipekee. "Tuligundua watu wakiruka upimaji afya ili kuuza bidhaa, kwa hivyo tuliteua madaktari ndani ya treni kutoa huduma bila malipo mara kwa mara," Xiang Baolin, kondakta mkuu wa treni hiyo ameeleza.
Xiang, mwenye umri wa miaka 59, amekuwa akifanya kazi kwenye njia hiyo ya treni tangu mwaka 1987 na ameshuhudia mabadiliko yaliyotokea kwenye treni hiyo moja kwa moja.
Xiang amekumbuka kwamba siku za nyuma, moshi wa makaa ya mawe ulisonga mabahewa ya treni hiyo wakati wa majira ya baridi, wakati wa majira ya joto, feni zenye kutu zilichochea hewa yenye kunata. Makondakta kama yeye walilazimika kutayarisha milo ya siku mbili kwa kila usafiri kwa kuwa hakukuwa na behewa la chakula ndani ya treni hiyo.
Katika miaka mingi iliyopita, kadri treni hiyo ilivyoboreshwa -- ikiongezwa mfumo wa joto, viyoyozi, na huduma nyingine - jukumu la Xiang pia limebadilika. Si tu kondakta sasa bali rafiki.
Abiria humwalika kwenye harusi, kumwelezea habari za mafanikio yao ya maisha na hata kumtumia ujumbe baada ya siku ya soko yenye mafanikio. "Wao ni kama familia," amesema.
Katika njia hiyo, shughuli mbalimbali zimekuwa zikistawi katika miaka mingi iliyopita, ikiwa ni pamoja na utalii wa kilimo na mashamba ya chai yanayoendeshwa kwa teknolojia.
Mbali na treni hizo za polepole, uboreshaji wa miundombinu, hasa upanuzi wa mitandao ya reli ya mwendo kasi, pia unachangia kuharakisha ustawishaji vijijini.
Ingawa mtandao wa reli za mwendo kasi unaozidi kuwa mpana umeimarisha muunganisho wa jamii za vijijini, treni hizo za mwendo wa polepole za nauli chini kama Na. 6064 bado zitaendelea kutoa huduma.
Xiang Baolin, Kondakta Mkuu wa treni Na. 6064 (kushoto), akizungumza na abiria nje ya Stesheni ya Reli ya Yanzibian katika Mkoa wa Shaanxi, kaskazini-magharibi mwa China, Februari 17, 2025. (Xinhua/Shao Rui)
Abiria akipanga mboga za majani ndani ya treni Na. 6064 (kushoto), inayoendeshwa kutoka Guangyuan katika Mkoa wa Sichuan, kusini-magharibi mwa China hadi Baoji katika Mkoa wa Shaanxi, kaskazini-magharibi mwa China, Februari 17, 2025. (Xinhua/Shao Rui)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma