

Lugha Nyingine
Ukraine yakubali usimamishaji mapigano kwa siku 30 kwenye mazungumzo na Marekani nchini Saudi Arabia
Wajumbe wa Marekani na Ukraine wakikutana mjini Jeddah, Saudi Arabia, Machi 11, 2025. (Xinhua/Wang Dongzhen)
JEDDAH, Saudi Arabia - Ukraine imeashiria utayari wake wa kukubali pendekezo la Marekani la "usimamishaji mapigano wa muda wa siku 30, mara moja" kufuatia mazungumzo na ujumbe wa Marekani mjini Jeddah, Saudi Arabia, kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa jana Jumanne.
Taarifa hiyo iliyotolewa baada ya masaa kadhaa ya mashauriano kati ya maafisa waandamizi kutoka nchi hizo mbili, imesema muda wa usimamishaji mapigano huo unaweza kurefushwa kwa makubaliano ya pande zote mbili, ikiongeza kuwa "Marekani itawasilisha taarifa kwa Russia kwamba hatua sawa na hiyo kwa upande wa Russia ndiyo ufunguo wa kupatikana kwa amani."
Washington imekubali "kuondoa mara moja usitishaji juu ya mabadilishano ya taarifa za kiintelijensia na kuanza tena usaidizi wa kiusalama kwa Ukraine," imesema taarifa hiyo, ikiongeza kuwa pande zote mbili zimejadili umuhimu wa juhudi za misaada ya kibinadamu, haswa wakati wa usimamishaji mapigano.
Wapatanishi pia wamekubaliana kuteua timu ya kuanza mazungumzo yenye lengo la kufikia amani ya kudumu. Marekani imesisitiza tena dhamira yake ya kuwasiliana na wawakilishi wa Russia, huku Ukraine ikisisitiza haja ya washirika wa Ulaya kuhusika katika mchakato huo, imesema taarifa hiyo.
Zaidi ya hayo, viongozi hao wa nchi hizo mbili wamekubaliana kukamilisha "mapema iwezekanavyo makubaliano ya kina ya kuendeleza rasilimali muhimu za madini ya Ukraine ili kupanua uchumi wa Ukraine," imeongeza.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio (katikati), Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani Mike Waltz (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan Al Saud wakiwa katika picha kwenye mkutano wa ngazi ya juu mjini Jeddah, Saudi Arabia, Machi 11, 2025. (Xinhua/Wang Dongzhen)
Tangazo hilo limefuatia mkutano wa ngazi ya juu uliohudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Mareakni Mike Waltz.
Ujumbe wa Ukraine ulijumuisha Mkuu wa Ofisi ya Ikulu ya Ukraine Andriy Yermak, Waziri wa Mambo ya Nje Andrii Sybiha, Waziri wa Ulinzi Rustem Umerov, na wengine. Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan Al Saud na Mshauri wa Usalama wa Taifa wa nchi hiyo Musaed bin Muhammad Al-Aiban pia wameshiriki katika majadiliano hayo.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari kufuatia mazungumzo hayo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio ameeleza matazamio kuwa Russia itakubali pendekezo hilo la kusimamisha mapigano kwa muda na Ukraine.
Amesema ahadi hiyo ya Ukraine "itawasilishwa kwao moja kwa moja kupitia njia nyingi," "kupitia njia zetu za kidiplomasia, kupitia mazungumzo, na njia zingine."
"Mpira uko kwenye uwanja wao," Rubio amesema, akibainisha kuwa kama Kremlin itakataa pendekezo hilo, "basi, kwa bahati mbaya, tutajua kizuizi cha amani ni kipi hapa."
Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman (kulia mbele) akimkaribisha Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mjini Jeddah, Saudi Arabia, Machi 10, 2025. (SPA/Kitini kupitia Xinhua)
Zelensky ameuelezea mkutano huo kuwa "mzuri na wa kiujenzi" kwenye mtandao wa kijamii wa X. "Kama Russia itakubali, usimamishaji mapigano utaanza kutekelezwa mara moja," Zelensky amesema.
Rais wa Marekani Donald Trump amesema anatarajia kuzungumza na Rais wa Russia Vladimir Putin baadaye wiki hii na anatumai Russia pia itakubaliana na makubaliano hayo.
Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman Al Saud (Kulia) akikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio mjini Jeddah, Saudi Arabia, Machi 10, 2025. (Shirika la Habari la Saudia/kupitia Xinhua)
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Russia, Dmitry Peskov, msemaji wa Rais Putin, amesema Moscow inatarajia Washington kutaarifu kuhusu mazungumzo hayo na Ukraine, akisisitiza kwamba kusiwe na kusherehekea kwa mapema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma