

Lugha Nyingine
Afrika Kusini kutumia dola za Kimarekani zaidi ya bilioni 54 kwa miundombinu katika miaka 3 ijayo
Waziri wa Fedha wa Afrika Kusini Enoch Godongwana akitoa Hotuba ya Bajeti ya mwaka 2025 bungeni mjini Cape Town, Afrika Kusini, Machi 12, 2025. (Picha na Xabiso Mkhabela/Xinhua)
CAPE TOWN - Afrika Kusini imetangaza mpango wa miaka mitatu wa kutumia randi zaidi ya trilioni 1 (dola za Kimarekani karibu bilioni 54.5) kwa miundombinu ya umma ili kukuza uchumi.
Waziri wa Fedha wa nchi hiyo Enoch Godongwana ametoa tangazo hilo wakati akiwasilisha mapitio ya Bajeti ya Mwaka 2025 na kutoa hotuba yake ya mwaka ya bajeti bungeni mjini Cape Town, mji mkuu wa kibunge wa nchi hiyo.
Godongwana ameeleza vipaumbele vya matumizi ya serikali baada ya uwasilishaji bajeti hiyo kuahirishwa kwa wiki tatu kutokana na kukosekana kwa makubaliano ya ndani kuhusu mapendekezo ya ongezeko la kodi ya thamani (VAT).
"Miundombinu ni nguzo muhimu ya mkakati wetu wa ukuaji. Ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi, chanzo kikuu cha ajira na njia ya kuongeza utoaji wa huduma," amesema Godongwana.
"Bajeti hii inaakisi uelewa huo. Mgao wa malipo ya mtaji ndiyo eneo linalokua kwa kasi zaidi la matumizi kwa uainishaji wa kiuchumi. Matumizi kwenye miundombinu ya umma katika kipindi cha miaka mitatu ijayo yatafikia randi zaidi ya trilioni 1," amesema.
Kwa mujibu wake, mgao wa fedha kwa ajili ya miundombinu utaelekezwa kwenye sekta kuu tatu, zikiwemo randi bilioni 402 kwa ajili ya usafirishaji na uchukuzi, randi bilioni 219.2 kwa miundombinu ya nishati, na randi bilioni 156.3 kwa maji na usafi wa mazingira.
Waziri huyo amezungumzia kwa msisitizo baadhi ya miradi muhimu ambayo itakuwa ikitekelezwa. "Katika usafiri, Shirika la Taifa la Barabara la Afrika Kusini litatumia randi bilioni 100 katika muda wa kati kuweka mtandao wa barabara wa taifa katika hali nzuri," Godongwana amesema.
Wakati huo huo, Shirika la Reli la Abiria la Afrika Kusini limetengewa kwa muda randi bilioni 19.2 kwa ajili ya uboreshaji wa alama muhimu. Katika sekta ya maji, miradi kadhaa mikubwa ya mabwawa inaharakishwa au inakaribia awamu ya ujenzi, amesema.
Katika hotuba yake hiyo, Godongwana pia amesema kuwa uchumi wa Afrika Kusini umekuwa kwenye mdororo kwa zaidi ya muongo mmoja, huku ukuaji wa Pato la Taifa ukiwa chini ya asilimia 2, chini ya kile kinachohitajika kwa kukidhi mahitaji ya nchi hiyo yanayopanuka.
"Mwaka 2024, uchumi ulikua kwa asilimia 0.6 tu," amesema, akiongeza kuwa ukuaji wa Pato la Taifa "unakadiriwa kuwa wastani wa asilimia 1.8" katika kipindi cha kati, ambacho ni miaka mitatu kutoka 2025 hadi 2027.
Kwa mujibu wa Godongwana, matumizi ya pamoja ya Serikali, bila kujumuisha malipo ya riba, yanatarajiwa kuongezeka kutoka randi trilioni 2.4 katika mwaka wa fedha wa 2024/25 hadi randi trilioni 2.83 mwaka wa 2027/28.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma