Zimbabwe yatafuta kuimarisha ushirikiano wa mazingira na China

(CRI Online) Machi 13, 2025

Waziri wa Habari, Mawasiliano ya Umma na Huduma za Utangazaji wa Zimbabwe Jefan Muswere amesema, nchi hiyo inatafuta kuimarisha ushirikiano wa mazingira na China.

Akizungumza siku ya Jumanne kwenye mkutano na waandishi wa habari wa baada ya kikao cha baraza la mawaziri la nchi hiyo, Muswere amesema ziara ya Waziri wa Mazingira, Tabianchi na Wanyamapori wa nchi hiyo Sithembiso Nyoni nchini China mwezi uliopita ililenga kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika sekta ya mazingira.

Kwa mujibu wa tovuti rasmi ya Mkataba wa Ramsar kuhusu Ardhi Oevu, Mkutano wa 15 wa Pande Watiasaini Mkataba wa Bioanuwai (COP 15) utafanyika kuanzia Julai 23 hadi 31 huko Victoria Falls nchini Zimbabwe.

Muswere amesema serikali ya Zimbabwe imechukua hatua kadhaa kuimarisha maandalizi ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo, akiongeza kuwa kamati ya mawaziri tayari imeanzishwa ili kuongoza kazi ya maandalizi.

Serikali ya Zimbabwe imesema itatumia mkutano huo kuongeza ushawishi na uongozi wake kwenye jukwaa la kimataifa katika usimamizi wa mazingira na mambo ya kidiplomasia.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha