

Lugha Nyingine
Ukubwa wa soko la uchumi wa barafu na theluji wafikia Yuan bilioni 266 Mkoani Heilongjiang, China
Watu wakifurahia mtelezo kwenye barafu katika Bustani ya dunia ya Barafu na Theluji ya Harbin mjini Harbin, Mkoa wa Heilongjiang, kaskazini mashariki mwa China, Februari 26, 2025. (Xinhua/Wang Jianwei)
HARBIN - Ukubwa wa soko la uchumi wa barafu na theluji katika Mkoa wa Heilongjiang, kaskazini-mashariki mwa China, ulikuwa umefikia yuan bilioni 266.17 (dola za Kimarekani karibu bilioni 37.1) katika kipindi cha mwaka 2024, ambapo kati yake pato la utalii wa barafu na theluji lilikuwa yuan bilioni 182.33, ofisi ya takwimu ya mkoa huo imesema.
Ofisi hiyo imesema kuwa, katika majira ya baridi ya 2024-2025, mkoa huo wa Heilongjiang ulipokea watalii milioni 135 wa ndani na nje ya nchi, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18.5 ikilinganishwa na msimu wa baridi wa mwaka jana. Aidha, matumizi kwenye utalii pia yaliongezeka kwa asilimia 30.7.
Mkoa huo umechukua uongozi kitaifa katika kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji kitakwimu kwa uchumi wa barafu na theluji mwaka huu. Katika kipindi cha miezi michache iliyopita, ofisi hiyo ilikusanya na kuchambua takwimu zinazohusiana na sekta hiyo kwa kushirikiana na idara za kodi, utalii wa kitamaduni, michezo, uchukuzi, kilimo na maeneo ya vijijini na viwanda na habari.
Ofisi hiyo pia ilifanya utafiti juu ya miradi zaidi ya 200 muhimu ya utalii katika kategoria saba ndani ya mkoa huo, ikijumuisha maeneo makubwa ya vivutio vya watalii, sehemu za manunuzi, maeneo maalum ya burudani za barafu na theluji, maeneo ya mapumziko ya michezo ya kuteleza kwenye barafu, makumbusho, majumba ya kitamaduni na sanaa, masoko ya asubuhi na usiku, ukihusisha wadau zaidi ya 40,000 wa biashara.
"Takwimu zilionyesha kikamilifu matokeo ya maendeleo ya Heilongjiang kama mahali pa kutekeleza wazo kwamba 'barafu na theluji pia ni mali muhimu sana'," amesema Yan Huijun, naibu mkuu wa ofisi hiyo.
China imezindua mpango kabambe wa kuendeleza uchumi wake wa barafu na theluji kama kichocheo kipya cha uchumi, ikilenga soko la jumla la Yuan trilioni 1.2 ifikapo mwaka 2027 na yuan trilioni 1.5 ifikapo mwaka 2030, kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na Baraza la Serikali la China mwaka 2024.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma