

Lugha Nyingine
M23 yaondoa ushiriki wake katika mazungumzo ya moja kwa moja na serikali ya DRC
KINSHASA - Mazungumzo na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), yaliyokuwa yamepangwa kufanyika leo Jumanne mjini Luanda, mji mkuu wa Angola, "yamekuwa yasiyowezekana," kundi la waasi la Vuguvugu la Machi 23 (M23) limesema katika taarifa yake iliyotolewa jana Jumatatu.
Mambo bado yanaendelea kujitokeza katika maandalizi ya mazungumzo yaliyopangwa na kutarajiwa ya moja kwa moja kati ya serikali ya DRC na waasi hao wa M23 siku ya Jumanne mjini Luanda. Rais wa Angola Joao Lourenco, mdau muhimu katika Mchakato wa Luanda, mfumo wa amani unaoungwa mkono na Umoja wa Afrika (AU), aliongoza mazungumzo hayo.
"Vikwazo mbalimbali vilivyowekwa kwa watu wetu, vikiwemo vile vilivyopitishwa katika usiku wa kuamkia mazungumzo ya Luanda, vinaathiri kwa kiasi kikubwa mazungumzo hayo ya moja kwa moja na kufanya upigaji hatua wowote kutowezekana," M23 imesema, ikirejelea vikwazo vilivyotangazwa Jumatatu na Umoja wa Ulaya dhidi ya baadhi ya viongozi wa M23 na makamanda wa kijeshi wa Rwanda, akiwemo kiongozi wa kisiasa wa M23 Bertrand Bisimwa.
Tina Salama, msemaji wa Rais wa DRC, ameviambia vyombo vya habari kwamba ujumbe wa DRC, ambao ulitakiwa kuondoka kuelekea Luanda siku hiyo ya Jumatatu jioni, bado ungefunga safari hiyo licha ya M23 kutokuonekana.
"Ujumbe wa DRC hakika utaitikia mwaliko wa mpatanishi, Rais Lourenco, mjini Luanda Jumanne hii," amesema Salama.
DRC imekuwa ikiishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi hilo la M23, huku Rwanda ikisema Jeshi la DRC limeshirikiana na kundi la waasi wa Rwanda la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda, ambalo linashutumiwa kuhusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
M23 ilitoa wito hapo awali kwa Rais wa DRC Felix Tshisekedi kutoa tamko la wazi kujitolea kufanya mazungumzo hayo ya moja kwa moja. Serikali ya DRC mara kwa mara imekuwa ikichukulia kama mstari mwekundu kuketi katika meza moja ya mazungumzo na waasi hao, ambao wameteka sehemu kubwa ya ardhi katika majimbo ya mashariki ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
Katika majimbo hayo, Muungano wa Mto Kongo (AFC), kikundi cha kisiasa na kijeshi kinachoshirikiana na M23, kimeanzisha utawala sambamba wa kijimbo.
"Kamwe, haitakuja kutokea, ilimradi mimi ni rais wa DRC, kuja kuwa mbele yangu na ujumbe wa M23 au AFC huko ... kufanya mazungumzo," Tshisekedi alisema katika mahojiano Agosti 2024.
Rwanda siku ya Jumatatu ilikata uhusiano wake wa kidiplomasia na Ubelgiji na kuamuru wanadiplomasia wake wote wa Ubelgiji kuondoka nchini humo ndani ya saa 48.
"Ubelgiji mara kwa mara imekuwa ikiidhoofisha Rwanda, kabla na wakati wa mgogoro huo unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo Ubelgiji ina nafasi ya kina ya kihistoria na kimabavu, haswa katika kuchukua hatua dhidi ya Rwanda," wizara ya mambo ya nje ya Rwanda imesema katika taarifa yake.
Mapigano yanayoendelea katika pande nyingi za DRC, yakichochewa na kuendelea kwa mashambulizi ya M23, yanatishia kuenea na kuwa mgogoro mkubwa zaidi wa kikanda. "Kama itaendelea namna hii, vita vinaweza kuenea katika kanda," Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye alionya mapema Februari.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma