

Lugha Nyingine
Trump na Putin wakubaliana "kusimamisha vita kwenye maeneo ya nishati na miundombinu" nchini Ukraine
Picha ya kuunganisha ikimuonyesha Rais wa Marekani Donald Trump (kushoto) na mwenzake wa Russia Vladimir Putin. (Xinhua)
WASHINGTON - Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Russia Vladimir Putin wamekubaliana kwa njia ya simu jana Jumanne kwamba amani nchini Ukraine "itaanza kwa kusimamisha vita kwenye maeneo ya nishati na miundombinu."
Wakati huo huo, wamekubaliana "mara moja" kuanzisha mazungumzo ya kiufundi juu ya kutekeleza usimamishaji vita baharini katika Bahari Nyeusi, vile vile juu ya usimamishaji wa vita kwa pande zote na amani ya kudumu nchini Ukraine, Ikulu ya White House imesema katika taarifa yake.
"Mazungumzo haya yataanza mara moja Mashariki ya Kati," imesema taarifa hiyo, ikibainisha kuwa viongozi hao wawili wamekubaliana kwamba mgogoro huo wa miaka mitatu nchini Ukraine unahitaji kumalizika kwa amani ya kudumu.
Viongozi hao wawili wamesisitiza haja ya kuboreshwa kwa uhusiano kati ya Marekani na Russia, imesema taarifa hiyo. Maelezo zaidi ya makubaliano hayo hayapatikani mara moja, lakini vyombo vya habari vya Marekani, vikitoa rejea kwa vyanzo vya habari nchini Russia, vimesema wamekubaliana kurejesha uhusiano kati ya nchi hizo mbili kwenye hali ya kawaida.
Haijafahamika mara moja jibu la Ukraine kwa mpango huo wa kusimamisha vita. Awali, Ukraine ilisema iko tayari kukubali pendekezo la kusimamisha vita kwa siku 30 lililotolewa na Trump.
Kabla ya mazungumzo hayo kwa njia ya simu, Trump alisema, "Vipengele vingi vya Makubaliano ya Mwisho vimeshakubaliwa, lakini mambo mengi bado yanabaki."
Mambo juu ya Ukraine "kwa hakika hayatatatuliwa kwa njia ya simu, kama kweli itatatuliwa," mchambuzi wa Kituo cha Habari cha Marekani cha Fox News amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma