

Lugha Nyingine
Marekani yafanya raundi mpya ya mashambulizi ya anga kwenye mji mkuu wa Yemen na mikoa mingine
Picha iliyopigwa kwa simu janja Machi 19, 2025 ikionyesha moshi na moto vikifuka kutoka kwenye eneo la makazi kufuatia shambulizi la anga mjini Sanaa, Yemen. (Str/Xinhua)
SANAA – Raundi mpya ya mashambulizi ya anga ya Marekani yamepiga mji mkuu wa Yemen, Sanaa jana Jumatano jioni, yakisababisha watu takriban tisa kujeruhiwa, wakiwemo wanawake saba na watoto wawili, kwa mujibu wa televisheni ya al-Masirah inayomilikiwa na Kundi la wanangambo Wahouthi, ambapo mashambulizi hayo yameripotiwa kulenga jengo linaloendelea kujengwa katika eneo la makazi ya Geraf la Sanaa, yakiharibu majengo ya makazi ya karibu na kujeruhi raia waliokuwa wamejihifadhi katika jengo la karibu.
Shambulizi hilo ni shambulizi la pili la Marekani katika eneo hilo tangu Jumamosi, wakati mashambulizi ya awali yaliposababisha vifo vya watu 53 na kujeruhi 98, wakiwemo wanawake na watoto, kwa mujibu wa mamlaka ya afya inayodhibitiwa na Wahouthi.
Mashambulizi hayo ya jana Jumatano pia yalipanuka katika maeneo mingine, huku al-Masirah ikiripoti mashambulizi katika maeneo yanayodhibitiwa na Wahouthi katika mikoa kama vile Saada, al-Bayda, Hodeidah na al-Jawf.
Waasi hao wa Houthi, ambao wanadhibiti eneo la kaskazini mwa Yemen, walidai mapema siku hiyo ya Jumatano kuwa walirusha makombora kwenye Manowari ya Marekani ya USS Harry Truman katika Bahari Nyekundu, wakilielezea kuwa shambulizi lao la nne la namna hiyo katika muda wa saa 72.
Kundi hilo linasisitiza kuwa mashambulizi yake ya baharini yanalenga meli zenye uhusiano na Israel pekee ili kuishinikiza Israel kusitisha mashambulizi yake katika Gaza na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia katika eneo hilo la Palestina.
Jeshi la Marekani, ambalo lilianza kushambulia maeneo lengwa ya Wahouthi Jumamosi, linasema operesheni hiyo inalenga kulinda njia za kimataifa za meli.
Rais wa Marekani Donald Trump amewaonya Wahouthi siku ya Jumamosi kusitisha mashambulizi hayo la sivyo watakabiliwa na madhara makubwa, akitangaza, "Jehanamu itawanyeshea kwa namna ambayo hamjawahi kushuhudia kabla."
Picha iliyopigwa kwa simu janja Machi 19, 2025 ikionyesha moshi na moto vikifuka kutoka kwenye eneo la makazi kufuatia shambulizi la anga mjini Sanaa, Yemen. (Str/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma