

Lugha Nyingine
Mazungumzo kati ya DRC na M23 yafutwa, juhudi za kutafuta amani zaendelea
(Photo na Camille Laffont/CFP)
KINSHASA/LUANDA - Kundi la waasi la Vuguvugu la Machi 23 (M23) kwa maamuzi ya upande mmoja limefuta mkutano uliopangwa wa mazungumzo ya moja kwa moja na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), likilaumu vikwazo vya Umoja wa Ulaya (EU) kama kizuizi. Juhudi za upatanishi za kikanda zimekwama kwani miito ya kusimamisha mapigano bado haijaleta matokeo katika maeneo yenye vita.
M23 kurudi nje
Mazungumzo hayo na serikali ya DRC, yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Jumanne mjini Luanda, mji mkuu wa Angola, "yamekuwa yasiyotekelezeka," M23 ilisema katika taarifa yake Jumatatu jioni.
Mkutano huo wa moja kwa moja uliotarajiwa sana kati ya serikali ya DRC na waasi hao wa M23 ulikuwa umeratibiwa na Rais Joao Lourenco wa Angola, mpatanishi mkuu katika Mchakato wa Luanda, utaratibu wa amani unaoungwa mkono na Umoja wa Afrika (AU).
"Masharti yote yameafikiwa kwa mazungumzo kuanza Machi 18, kama ilivyopangwa," rais huyo wa Angola alisema Jumatatu jioni, akiongeza kuwa ujumbe wa serikali ya DRC tayari ulikuwa umewasili Luanda, huku ujumbe wa M23 ulikuwa ukitarajiwa baadaye.
Hata hivyo, Jumanne jioni, Wizara ya Mambo ya Nje ya Angola ilisema mazungumzo hayo yalikuwa yamefutwa kutokana na "sababu na mazingira yaliyo nje ya uwezo."
Kulaumu vikwazo vya EU
Kundi la M23 lilisema kuwa "baadhi ya taasisi za kimataifa" zinajaribu kwa makusudi kuhujumu juhudi za amani nchini DRC na kukwamisha mazungumzo hayo, likirejelea vikwazo vilivyowekwa kwa viongozi wake, vikiwemo vile vilivyopitishwa katika usiku wa kuamkia wa mazungumzo hayo ya Luanda.
Siku ya Jumanne, Jean-Marc Chataigner, balozi wa zamani wa Umoja wa Ulaya nchini DRC, alikanusha maelezo hayo ya M23 ya kurudi nje ya mazungumzo hayo ya amani akiyaelezea kuwa ni kisingizio dhaifu.
"Hakuna uhusiano wowote! Vikwazo vya EU havijaizuia kwa vyovyote Angola kuwa mwenyeji wa ujumbe kutoka M23," Chataigner alisema.
Juhudi za upatanishi bado zinaendelea
Siku ya Jumatatu, jumuiya mbili za kikanda -- Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) -- ziliitisha mkutano wa mawaziri mjini Harare, mji mkuu wa Zimbabwe, kutafuta njia za kusimamisha mapigano kwa kudumu.
Mawaziri hao wamekubaliana kuchukua hatua za kujenga imani katika ngazi zote za kisiasa na kijeshi ndani ya mchakato uliounganishwa wa Luanda na Nairobi ili kufikia makubaliano ya kusimamisha mapigano kwa kudumu katika miezi michache ijayo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma