Tanzania yazindua Sera ya Taifa ya Maji toleo la 2025 ili kuimarisha ulinzi na upatikanaji wa maji

(CRI Online) Machi 24, 2025

Tanzania imezindua Sera ya Taifa ya Maji toleo la 2025, inayolenga kuongeza upatikanaji wa maji na kuimarisha ulinzi wa vyanzo vya maji.

Sera hiyo mpya, ikiwa ni maboresho ya toleo la 2002, imezinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan wa nchi hiyo jijini Dar es Salaam Jumamosi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani.

Rais Samia amesema sera ya maji iliyoboreshwa inaongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kufadhili miradi ya maji na kuimarisha ulinzi wa miundombinu ya maji ili kuimarisha upatikanaji wa maji.

Mkuu huyo wa nchi amesisitiza kwamba ulinzi wa vyanzo vya maji si jukumu la Wizara ya Maji pekee, bali ni la Watanzania wote.

Alitoa wito wa kuunda gridi ya taifa ya maji ili kusimamia matumizi ya rasilimali za maji nchini kote, huku akihimiza wananchi wenzake kujenga tabia ya kuvuna maji ya mvua kwa ajili ya matumizi wakati rasilimali hiyo ni adimu.

Naye Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe, Nathan Belete, ameipongeza Tanzania kwa uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Maji ya 2025, akisema toleo hilo jipya linalenga kuhakikisha maendeleo bora, endelevu, ya kuaminika na yenye usawa, na matumizi ya rasilimali ya maji kwa manufaa ya wote na kwa gharama nafuu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha