

Lugha Nyingine
Rwanda yakaribisha waasi wa M23 kuondoka kutoka mji wa Walikale mashariki mwa DRC
KIGALI – Rwanda imekaribisha uamuzi wa kundi la waasi wa Vuguvugu la Machi 23 (M23) kuondoka kutoka mji wa Walikale, ambao liliuteka mwanzoni mwa wiki, na pia imekaribisha uamuzi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kupunguza uhasama mashariki mwa DRC.
Muungano wa Mto Congo, ambao ni shirikisho la kisiasa na kijeshi linalojumuisha waasi wa M23, ulitangaza Jumamosi uamuzi wake wa "kuvipanga upya" vikosi vyake kutoka Walikale na maeneo jirani. Umesema, hatua hiyo inalenga kuunga mkono juhudi za amani na kuweka mazingira mwafaka kwa mazungumzo ya kisiasa ili kushughulikia sababu kuu za mgogoro huo wa mashariki mwa DRC.
Kwa kujibu uamuzi huo , Jeshi la DRC lilivihimiza vikosi vya kujilinda vya DRC kuacha mashambulizi siku hiyo hiyo, likisisitiza haja ya kuzingatia kwanza kufanya mazungumzo ya amani na kusukuma mbele mchakato wa mazungumzo ya Luanda na Nairobi.
Taarifa kutoka kwa ofisi ya msemaji wa serikali ya Rwanda iliyotolewa siku ya Jumapili imesema: "Rwanda inakaribisha uamuzi wa M23 kuhusu kuvipanga upya vikosi vyake kutoka Walikale ili kuunga mkono juhudi za amani zinazoendelea, na pia inakaribisha serikali ya DRC kutangaza kusitisha operesheni zote za mashambulizi za FARDC (vikosi vya serikali ya DRC) na Wazalendo (wanamgambo wanaoiunga mkono serikali)."
"Rwanda imedhamiria kufanya ushirikiano na pande zote ili kuhakikisha inatimiza ahadi yake, hasa katika muktadha wa mchakato wa pamoja wa mkutano wa kilele wa EAC-SADC na jitihada nyingine zinazoandaa njia kwa ajili ya suluhu ya kudumu ya kisiasa na kiusalama katika kanda," imesema taarifa hiyo.
Tangu kuzidisha mashambulizi yake mwaka jana, kundi hilo la waasi la M23 limeteka maeneo makubwa katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini mashariki mwa DRC.
Nchi ya DRC imekuwa ikiilaumu Rwanda kuunga mkono kundi hilo, madai ambayo Kigali imekuwa ikiyakanusha. Kwa upande wake, Rwanda imekuwa ikililaumu jeshi la DRC kushirikiana na kundi la waasi la Rwanda la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda, ambalo linashutumiwa kuhusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Siku ya Jumanne wiki iliyopita, Rais wa DRC Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame walitoa wito wa kusimamisha mapigano kwenye mkutano wa dharura mjini Doha, Qatar, hii ni mara ya kwanza kusimamisha mapigano tangu M23 kuteka miji mikuu ya Goma na Bukavu ya majimbo hayo mwaka huu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma