Polisi wa Uturuki wakamata watu zaidi ya 1,400 katika maandamano ya kupinga kuzuiliwa kwa meya wa Istanbul

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 26, 2025

ANKARA - Vikosi vya usalama vya Uturuki vimekamata washukiwa 1,418 tangu kuanza kwa maandamano ya kupinga kuzuiliwa kwa Meya wa Jiji la Istanbul Ekrem Imamoglu wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo Ali Yerlikaya amesema Jumanne.

Kwa sasa kuna washukiwa 979 walio kizuizini, huku watu 478 watapelekwa kwa mamlaka za mahakama, Yerlikaya amesema kupitia ujumbe wake uliochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Wakati huo huo, Ozgur Ozel, mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani cha Republican People's Party (CHP), amesema atahitimisha maandamano yake katika wilaya ya Sarachane ya Istanbul kufikia jana Jumanne jioni.

Makumi ya maelfu ya Waturuki wamekuwa wakiingia mitaani tangu Machi 19 baada ya Imamoglu kuzuiliwa kwa tuhuma za ufisadi na uhusiano wa kigaidi. Imamoglu, kutoka CHP, anachukuliwa kuwa mpinzani mkuu wa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika uchaguzi ujao wa urais.

Rais Erdogan Jumatatu alikilaumu chama cha CHP kwa maandamano hayo ya sasa ya nchini ambayo yameongezeka hadi kufikia kile alichokiita "vuguvugu la kimabavu," akisema CHP na waungaji mkono wake wanapaswa kuwajibika kwa "maafisa wa polisi waliojeruhiwa, maduka yaliyoharibiwa, na mali ya umma iliyoharibiwa."

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha