

Lugha Nyingine
Rais wa Afrika Kusini aonya dhidi ya "siasa za migawanyiko" wakati balozi aliyefukuzwa Marekani akirejea
Picha hii iliyopigwa Agosti 10, 2023 ikionyesha maandhari ya Johannesburg, Afrika Kusini. (Xinhua)
JOHANNESBURG - Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amehimiza raia wa nchi hiyo kukataa "siasa za migawanyiko" kutoka sehemu nyingine za dunia, kufuatia kuwasili kwa Ebrahim Rasool, balozi wa nchi hiyo aliyefukuzwa kutoka nchini Marekani.
"Tunapaswa kupinga kauli potofu kabisa kwamba nchi yetu ni mahali ambapo watu wa rangi au tamaduni fulani wanalengwa kwa mateso," amesisitiza katika taarifa yake ya kila wiki kwa taifa juzi Jumatatu.
Ramaphosa amesisitiza kwamba madai yanayotolewa na makundi fulani ya watu kwamba yanatendewa vibaya lazima yakataliwe. "Nchini Afrika Kusini leo, raia wote, Waafrika, Wazungu, Wahindi na watu wa rangi mbalimbali, wanaume na wanawake, wana haki sawa na uhuru ambao serikali inawajibika kuudumisha, kuulinda na kuuendeleza," amesema.
Ujumbe huo umekuja wakati Afrika Kusini hivi karibuni ikiadhimisha Siku ya Haki za Kibinadamu, ambayo inaadhimisha Mauaji ya Sharpeville ya Machi 21, 1960, wakati polisi wa ubaguzi wa rangi walipoua waandamanaji 69 wasio na silaha.
Ingawa Ramaphosa hakutaja nchi au viongozi wowote mahsusi, ukosoaji wa serikali ya Afrika Kusini umetoka kwa wanasiasa wa Marekani, akiwemo Rais Donald Trump. Hilo lilifikia kilele kwa Trump kutia saini amri tendaji kuwapa watu wa Kabila la Waafrikana hadhi ya ukimbizi nchini Marekani.
Balozi wa Afrika Kusini aliyefukuzwa kutoka nchini Marekani Ebrahim Rasool akizungumza na umati katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cape Town, Afrika Kusini, Machi 23, 2025. (Picha na Shakirah Thebus/Xinhua)
Rasool aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cape Town siku ya Jumapili. Alitarajiwa kusafiri hadi Pretoria, mji mkuu wa kiutawala wa Afrika Kusini, siku ya Jumatatu kukutana na Waziri wa Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini Ronald Lamola.
Idara ya Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini ilitoa taarifa Jumatatu kuhusu mkutano huo. Idara hiyo pia ilieleza kuwa ripoti rasmi itawasilishwa kwa rais ili kupitishwa, na kwamba suala hilo halitajadiliwa hadharani.
"Kabla ya kupitishwa, wizara au idara haitajihusisha na mazungumzo ya hadharani juu ya suala hilo," ilisema taarifa hiyo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma