

Lugha Nyingine
Kenya yawatunuku washindi 15 wa kambi ya mafunzo ya usalama mtandaoni inayoungwa mkono na Huawei
Hafla ya mahafali na utoaji tuzo kwa wahitimu 15 wa kambi ya nne ya mafunzo ya usalama mtandaoni kitaifa, inayoungwa mkono na kampuni ya mawasiliano ya China ya Huawei, imefanyika jijini Nairobi nchini Kenya jana Jumatano.
Naibu afisa mtendaji mkuu wa Huawei Kenya, Steven Zhang, amesema kampuni hiyo imeimarisha ushirikiano wake na sekta ya umma na akademia ili kukuza kizazi kijacho cha wataalamu wa mtandao wenye jukumu la kulinda miundombinu ya kidijitali nchini humo.
Zhang amesema kupitia ushirikiano na Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA), na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali ya Kenya, Huawei imeunga mkono kampeni ya 2025 ya kambi ya mafunzo ya usalama wa mtandaoni, ambayo ilipokea zaidi ya maombi 3,000.
Amebainisha kuwa ushirikiano wa kimkakati na mashirika ya serikali umekuwa muhimu katika kufanya mtandao wa intaneti wa Kenya kuwa salama kupitia kutoa mafunzo na ushauri kwa vijana wanaosomea kozi zinazohusiana na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika vyuo vya elimu ya juu.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na maafisa waandamizi wa serikali, watendaji wa sekta hiyo, washiriki wa kitivo, wanafunzi na wadau wa teknolojia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma