Wataalam wakutana nchini Kenya kuboresha biashara ya nje ya maua kutoka Afrika

(CRI Online) April 01, 2025

Wataalamu wa kilimo cha maua barani Afrika wamekutana jijini Nairobi, Kenya, kujadili mikakati ya kuboresha mauzo ya nje ya maua kutoka barani humo, kuimarisha upatikanaji wa soko, na kuboresha mnyororo fanisi wa ugavi.

Mkutano huo wa siku mbili wa Ugavi wa Maua wa mwaka 2025 umekutanisha maofisa wa ngazi ya juu wa serikali, watoa huduma za ugavi, wamiliki wa mashamba, wasafirishaji na viongozi wa viwanda kutoka barani Afrika, ambao wanatafuta njia za kuimarisha nafasi ya Afrika kama kiongozi wa mauzo ya maua duniani.

Ofisa Mkuu Mwandamizi katika Baraza la Maua la Kenya, Clement Tulezi amesema, changamoto kubwa inayokabili sekta ya maua barani Afrika ni kuongezeka kwa gharama za usafiri wa ndege kwa kuwa uwezo wa ndege za mizigo unabadilika kwa kufuata njia zenye faida zaidi.

Amesema Kenya, ambayo inaongoza kwa mauzo ya nje ya maua barani Afrika, inatafuta kuongeza mapato kutoka kwa sekta hiyo kwa kutafuta masoko mengine mapya kama China na Japan.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha