

Lugha Nyingine
Mabasi 100 yanayotumia umeme ya China yaingia mitaa ya mji mkuu wa Ethiopia
ADDIS ABABA - Serikali ya Jiji la Addis Ababa imeingiza mabasi 100 yanayotumia umeme katika sehemu mbalimbali za Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, ikiwa ni moja ya juhudi za kuhimiza usafiri wa magari yanayotumia umeme katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Yakiwa yameunganishwa sehemu zake na kampuni ya nchini humo ya Belayneh Kindie Metal Engineering Complex, huku vipuri vyake vikiwa vimeagizwa kutoka China, kundi hilo jipya la mabasi hayo yanayotumia umeme yenye vifaa vya Mfumo Jumuishi wa Usafiri wa Teknolojia za Kisasa na Mfumo wa Ukusanyaji Nauli, Shirika la Utangazaji la Ethiopia limeripoti jana Jumanne.
Mabasi hayo yanayotumia umeme yameanza rasmi kutoa huduma ya usafiri kirahisi kwa wakazi wa jiji hilo kwenye Njia ya Usafiri wa Haraka wa Mabasi, njia mpya ya usafiri wa umma katika jiji hilo.
"Mabasi haya yanayotumia umeme yataimarisha mtandao wa usafiri wa umma katika mji mkuu. Ni rafiki kwa mazingira yakiwa na utoaji sifuri wa hewa chafu na yanatoa usafiri mzuri wenye uwezo wa kutosha kwa abiria," Waziri wa Uchukuzi na Usafirishaji wa Ethiopia Alemu Sime amenukuliwa akisema.
Ameongeza kuwa mabasi hayo yanayotumia umeme yanaendeshwa kwenye njia maalum za mabasi ya kiumma, ili kuhakikisha usafiri wa haraka kwa wasafiri.
“Mabasi haya yanatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa upungufu wa usafiri wa umma jijini Addis Ababa na kutoa chaguo la usafiri wa umma mjini ulio wa starehe, ufanisi na endelevu zaidi kwa wakazi wake” amesema.
Wizara ya Uchukuzi na Usafirishaji ya Ethiopia imesema, magari zaidi ya 100,000 yanayotumia umeme kwa sasa yapo barabarani kote nchini humo, na serikali inalenga kuongeza idadi hiyo hadi kufikia magari 500,000 ndani ya muongo ujao, yakiwa mbadala wa asilimia 95 ya magari yanayotumia mafuta.
Wizara hiyo inasema, ili kuharakisha kuhamia matumizi ya magari yanayotumia umeme, serikali ya Ethiopia iliweka marufuku ya uagizaji magari ya petroli na dizeli mapema mwaka jana kutokana na kuongezeka kwa bei ya mafuta duniani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma