

Lugha Nyingine
Watu zaidi ya 33 wafariki baada ya mvua na mafuriko makubwa kukumba mji mkuu wa DRC
Picha hii iliyopigwa kwa simu ya mkononi ikionyesha watu wakitembea kwenye barabara iliyofurika maji huko Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Aprili 6, 2025. (Xinhua)
KINSHASA - Watu zaidi ya 33 wamefariki dunia kutokana na mvua kubwa na mafuriko makali huko Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), serikali imesema asubuhi ya Jumatatu.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama, Jacquemain Shabani, amesema mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia Ijumaa hadi Jumamosi imesababisha uharibifu mkubwa katika maeneo kadhaa ya mji mkuu, na kusababisha majeruhi kadhaa pamoja na kubomoa nyumba nyingi.
Ili kukabiliana na hali hiyo, serikali imeunda timu za usimamizi wa dharura kwa kushirikiana na jeshi, wizara kadhaa pamoja na serikali ya Kinshasa na kufanya shughuli za uokoaji na kupeleka vikosi vya dharura katika maeneo yaliyoathirika.
Mafuriko hayo yameathiri miundombinu mingi ya jiji hilo. Barabara kuu zilikuwa zimezama, ikisababisha kukatika kwa umeme na maji katika wilaya nyingi.
Wizara ya Uchukuzi ya DRC iliripoti usumbufu mkubwa wa njia za kuwezesha kufika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa N'djili, ikisababisha kuwekwa kwa huduma za dharura za feri kusaidia wasafiri waliokuwa wamekwama.
Utabiri wa hali ya hewa unasema mvuta kubwa utaendelea kunyesha katika siku kadhaa zijazo, ikiongeza hofu ya uharibifu zaidi katika jiji hilo la watu milioni 17, ambalo tayari liko katika hatari kwa sababu ya upanuzi wa mji ulio wa haraka na usiodhibitiwa.
Msimu wa mvua wa DRC kwa kawaida huanza Novemba hadi Mei.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma