

Lugha Nyingine
Msemaji wa Mambo ya Nje wa China afahamisha hali juu ya mawasiliano kati ya China na EU kuhusu ushuru wa Marekani
BEIJING - China inapenda kushirikiana na jumuiya ya kimataifa, ikiwemo Umoja wa Ulaya (EU), kulinda kwa pamoja utaratibu wa biashara wa kimataifa, haki na usawa, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Lin Jian amesema jana Jumatatu kwenye mkutano na waandishi wa habari alipoulizwa kuhusu hali ya mawasiliano na uratibu kati ya China na EU kuhusu ushuru wa ziada wa Marekani.
“Marekani inatumia ushuru kama silaha kutoa shinikizo kubwa na kutafuta faida binafsi, na kuweka maslahi yake yenyewe juu ya manufaa ya umma ya jumuiya ya kimataifa,” Lin amesema, akibainisha kuwa hii ni hatua halisi ya uamuzi wa upande mmoja, kujihami kibiashara na ukandamizaji wa kiuchumi, ambayo inaathiri vibaya maslahi ya China, Umoja wa Ulaya na dunia nzima.
Lin amesema kuwa China na Umoja wa Ulaya zikiwa makundi yenye uchumi wa pili na wa tatu kwa ukubwa duniani, zinachukua zaidi ya theluthi moja ya uchumi wa dunia na zaidi ya robo ya biashara ya kimataifa, akiongeza kuwa pande zote mbili ni watetezi wa utandawazi wa uchumi na biashara huria, na watetezi na waungaji mkono thabiti wa WTO.
"Mkuu wa EU alisisitiza umuhimu mkubwa wa utulivu na uhakika kwa maendeleo mazuri ya uchumi duniani. China na EU zimejitolea kwa kulinda mfumo wa biashara wa pande nyingi ulio wa haki, huria na unaozingatia WTO, na kuhimiza maendeleo mazuri na tulivu ya uhusiano wa kibiashara na kiuchumi duniani, ambayo inaendana na maslahi ya pande zote mbili na dunia nzima," Lin amesema.
Amesema, ikiwa nchi kubwa yenye kuwajibika, China tayari imechukua hatua madhubuti na itaendelea kufanya hivyo ili kulinda maslahi yake halali.
"China inapenda kushirikiana na jumuiya ya kimataifa, ikiwemo EU, kuimarisha mawasiliano na uratibu, kunufaisha pamoja fursa za maendeleo, kupanua ufunguaji mlango na ushirikiano, na kutimiza hali ya kunufaishana. Hatutalinda tu maslahi yenyewe, lakini pia kulinda utaratibu wa biashara za kimataifa, haki na usawa," Lin amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma