

Lugha Nyingine
China yaonesha kwa umma wanaanga wa chombo cha Shenzhou-20 watakaotekeleza jukumu la kituo cha anga ya juu
JIUQUAN - Wanaanga wa China Chen Dong, Chen Zhongrui na Wang Jie watatekeleza jukumu la safari ya chombo cha anga ya juu cha Shenzhou-20, na Chen Dong atakuwa kiongozi wao, Shirika la Anga ya Juu la China limetangaza Jumatano.
Chombo hicho cha anga ya juu cha Shenzhou-20 kimepangwa kurushwa leo Alhamisi saa 11:17 jioni (kwa saa za Beijing) kutoka Kituo cha Kurushia Satalaiti cha Jiuquan, kaskazini-magharibi mwa China, amesema Lin Xiqiang, msemaji wa shirika hilo, kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Picha hii iliyopigwa Aprili 16, 2025 ikionyesha chombo cha anga ya juu cha Shenzhou-20 na roketi ya kubeba ya Long March-2F kwa pamoja vikiandaliwa kuhamishiwa kwenye eneo la kurushia. (Picha na Wang Jiangbo/Xinhua)
Chen Dong amewahi kushiriki katika jukumu la chombo cha anga ya juu cha Shenzhou-11 na Shenzhou-14. Alikuwa kiongozi wa wanaanga wa chombo cha Shenzhou-14 na atachukua wadhifa huo kwa mara nyingine tena baada ya miaka miwili iliyopita. Na atakuwa mwanaanga atakayetekeleza kwa mara tatu majukumu ya chombo cha anga ya juu.
Chen Zhongrui na Wang Jie wote ni wa timu ya tatu ya wanaanga na wataanza kutekeleza jukumu lao la kwanza la anga ya juu.
Kabla ya kuchaguliwa, Chen Zhongrui alikuwa rubani wa ndege wa jeshi la anga la China, na Wang Jie alikuwa mhandisi katika Taasisi ya Teknolojia ya Anga ya Juu ya China chini ya Shirika la Sayansi na Teknolojia ya Anga ya Juu la China.
Chen Dong ameieleze timu yake ya wanaanga hao ni timu inayofanya kazi kwa usahihi na umakini mkubwa zaidi.
Akizungumza kwenye mkutano huo na waandishi wa habari wa jana Jumatano, Chen amesema rubani analeta fikra makini na ujuzi sahihi wa kiutendaji, huku mhandisi akichangia mwenendo wa kufanya kazi bila kulegalega hata kidogo na msingi thabiti wa kinadharia.
Chen Zhongrui anaelezewa na wanaanga wenzake kuwa mtulivu, makini na mwenye akili ya haraka. Akiwa rubani wa zamani, ana ujuzi bora wa uendeshaji.
Chen Zhongrui amewaambia waandishi wa habari kwamba mwanzoni mwa kufanya mazoezi ya pamoja, yeye na Wang Jie walihisi wasiwasi kidogo, kwani bado wakiwa wapya, na Chen Dong alikuwa tayari amekamilisha majukumu mawili ya anga ya juu. "Sasa, tunafanya kazi pamoja bila tatizo, na tunaona kama sisi ni mtu mmoja," amesema.
Wanaanga watakaotekeleza jukumu la safari ya chombo cha anga ya juu cha Shenzhou-20 Chen Dong (katikati), Chen Zhongrui (kulia) na Wang Jie wakikutana na waandishi wa habari kwenye Kituo cha Kurushia Satalaiti cha Jiuquan, kaskazini-magharibi mwa China tarehe 23 Aprili 2025. (Xinhua/Lian Zhen)
Wanaanga hao wapya watafanya kazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na majaribio ya sayansi ya anga ya juu, majaribio ya matumizi, shughuli za nje ya kituo cha anga ya juu, na kushughulikia mizigo. Jukumu lao pia linahusisha kufunga vifaa vya kujikinga na vifusi vya anga ya juu, na kuweka na kuchukua tena vitu na vifaa vya ziada.
Pia watashiriki katika elimu ya sayansi, uenezi kwa umma, na shughuli nyingine za majaribio ndani ya chombo.
Mfanyakazi akiangalia hali ya samakipundamili (zebrafish) kwa ajili ya matumizi ya ziada kwenye Kituo cha Kurushia Satalaiti cha Jiuquan, kaskazini-magharibi mwa China, Aprili 25, 2024. (Xinhua/Jin Liwang)
Lin Xiqiang, msemaji na naibu mkurugenzi wa Shirika la Anga ya Juu la China, akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusu jukumu la safari ya wanaanga wa chombo cha anga ya juu cha Shenzhou-20 kwenye Kituo cha Kurushia Satalaiti cha Jiuquan, kaskazini-magharibi mwa China, Aprili 25, 2024. (Xinhua/Bei He)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma