Wauzaji bidhaa nje wa Kenya wachukulia Soko la China kama mbadala ili kukabiliana na utozaji kodi ya juu wa Marekani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 27, 2025

Picha iliyopigwa Mei 31, 2023 ikionesha ukumbi wa Maonesho ya pili ya kimataifa ya Maparachichi ya Afrika (Avocado Africa 2023). (Picha/Xinhua)

Picha iliyopigwa Mei 31, 2023 ikionesha ukumbi wa Maonesho ya pili ya kimataifa ya Maparachichi ya Afrika (Avocado Africa 2023). (Picha/Xinhua)

Wauzaji bidhaa nje wa Kenya wanaichukua zaidi China kuwa soko mbadala na la kutegemewa kwa bidhaa zao ili kukabiliana na hali ya msukosuko unaozidishwa duniani kutokana na sera ya utozaji kodi ya Marekani ya hivi karibuni.

Maofisa wa serikali ya Kenya pamoja na wasimamizi wakuu wa kampuni za Kenya walisema kuwa China yenye idadi ya watu bilioni 1.4 na ongezeko la haraka la uchumi, ni soko kubwa kwa bidhaa za Kenya, hasa mazao ya kilimo.

"China ni soko kubwa kwa mazao yetu ya kilimo, lakini katika miaka mingi iliyopita, tumekuwa tukichukua nafasi ndogo tu kwenye soko hilo," alisema Floice Mukabana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Idara ya Uhimizaji wa Uuzaji Bidhaa Nje na Uenezaji wa Chapa ya Kenya. "Lengo letu ni kusambaza bidhaa zetu sehemu mbalimbali nchini China ili kila mtumiaji nchini China aweze kununua bidhaa zetu."

Maonesho ya Nne ya Uchumi na Biashara ya China na Afrika yatafanyika mwezi Juni mjini Changsha, China. Kwenye mkutano uliofanyika Nairobi kabla ya maonesho hayo, Mukabana alisisitiza kuwa, Kenya itatumia fursa ya maonesho hayo kupanua nafasi yake zaidi kwenye soko la China.

Josphine Ndikwe, mkurugenzi mkuu wa Biashara na Uuzaji wa Nje kutoka kampuni ya Jotim Coffee, alisema kuwa China ni soko zuri mbadala kwa Kenya, kwa sababu soko la China ni kubwa sana, na ushuru wake wa forodha siyo wa juu.

Alisema kampuni yake imekuwa ikiuza bidhaa nchini China tokea mwaka 2022, na uwezo wake wa uuzaji umeendelea kuongezeka kwa kiasi kikubwa.

"Tunatarajia kupanua soko letu na kuanzisha uuzaji wa kahawa iliyokaangwa, kwa kuwa tunaamini soko la China ni kubwa sana, na linapokea zaidi kahawa ya Kenya," alisema Ndikwe, akiongeza kuwa gharama ya kusafirisha bidhaa kwenda China ni ya chini kuliko zile za kwenda maeneo mengine.

Newton Ngure, Meneja Mkuu wa kampun ya uuzaji wa nje ya Camilco, alisema kuwa maparachichi ya Kenya yana nafasi kubwa sana kwenye soko nchini China, akidhihirisha kuwa kampuni hiyo inakadiriwa kuuza angalau tani 40 za parachichi kila mwezi nchini China.

"Tumepokea oda ya parachichi na kwa sasa tunajitahidi kupata cheti cha kusafirisha bidhaa kwenda China," alisema.

Simon Gakinya, Meneja Mkuu wa kampuni ya chai maalumu na kahawa ya Mount Kenya, alisema kuwa bidhaa za Kenya zina nafasi kubwa katika soko la China, akisema kuwa Wachina ni watu wenye urafiki na wachangamfu, na wanatarajia kufanya ushirikiano siku zote.

Gakinya alisema kuwa ili kuongeza uuzaji bidhaa za Kenya katika soko la China, serikali ya Kenya inapaswa kuweka sera zinazofaa ili kuwawezesha wafanyabiashara wa Kenya na China kukutana, kuelewana kuhusu utamaduni wa kila upande , njia ya uendeshaji wa biashara, na mapendeleo ya kila upande, , ili kuleta mafanikio kwa pande zote mbili.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha