

Lugha Nyingine
Sekta ya usafiri wa anga ya China kuongezeka wakati wa likizo ya Siku ya Wafanyakazi
Ndege inayoelekea Guangzhou, Mkoa wa Guangdong ikipaa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Tianshan mjini Urumqi, Mkoani Xinjiang, kaskazini-magharibi mwa China, Aprili 17, 2025. (Xinhua/Xu Hongyan)
BEIJING - Idadi ya abiria wanaosafiri kwa ndege nchini China inatarajiwa kuongezeka kwa kasi tulivu wakati wa likizo ijayo ya siku tano ya Siku ya Wafanyakazi Duniani huku idadi hiyo inakadiriwa kufikia milioni 10.75 kote nchini humo, kwa mujibu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya China (CAAC).
Likizo hiyo ambayo imepangwa kuanza Mei 1 hadi 5 inakadiriwa kushuhudia wastani wa safari za abiria milioni 2.15 kwa siku, ikiwa ni ongezeko la asilimia 8 ikilinganishwa na mwaka 2024 na kuweka rekodi mpya kwa kipindi hicho, Shang Kejia, afisa wa CAAC, amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari jana Jumapili.
Shang ameongeza kuwa siku za pilika za wasafiri wengi zinatarajiwa kufika katika siku za Mei Mosi na Mei 5 kwa watu milioni 2.3 kila moja.
Kwa mujibu wa afisa huyo, watu wanaosafiri zaidi ni katika njia kuu kati ya makundi manne muhimu ya miji ya China: Beijing-Tianjin-Hebei, Delta ya Mto Yangtze, Eneo la Ghuba Kuu ya Guangdong-Hong Kong-Macao, na Chengdu-Chongqing.
Aidha, ameeleza kuwa, safari kuelekea maeneo maarufu ya utalii, kama vile Xishuangbanna na Lijiang katika Mkoa wa Yunnan na Lhasa katika Mkoa wa Xizang, pia zitakuwa nyingi sana.
Shang ameeleza kuwa, usafiri wa kimataifa unatarajiwa kufikia kiwango chake cha juu zaidi tangu kuanza kwa robo ya pili, huku Japan, Korea Kusini, na nchi za Asia Kusini-Mashariki yakiendelea kuwa sehemu zitakazokwenda kwa watalii wengi zaidi.
CAAC imesisitiza kwamba sera za viza zilizorahisishwa kwa wasafiri wanaoingia China na wasafiri wanaounganisha ndege China kwenda nchi zingine, pamoja na huduma za kurejesha kodi, zinahimiza ongezeko la watalii wa kigeni wanaowasili na kuyafanya mashirika ya ndege ya kigeni kuongeza uwezo wa safari za ndege.
Imesema, ili kukidhi mahitaji makubwa ya usafiri, mashirika ya ndege yamepanga safari zilizo kwenye ratiba jumla ya 88,000 kwa ajili ya likizo hiyo, ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.3 ikilinganishwa na mwaka uliopita. Aidha, mipango ya usafiri wa ndege zaidi ya 173 imeidhinishwa, ikiwa ni ongezeko la asilimia 8 kuliko mwaka jana wakati kama huo.
Kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa, hali joto za juu zinatarajiwa nchi nzima wakati wa likizo hiyo, na kuongeza uwezekano wa hali ya hewa mbaya na mvua kubwa.
CAAC imehimiza idara zote za huduma za usafiri wa anga kuweka kipaumbele katika kukabiliana na hali mbalimbali za hewa, kutekeleza hatua za usalama, na kupunguza hatari za hali ya hewa mbaya.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma