

Lugha Nyingine
Idadi ya vifo katika mlipuko wa bandari ya kusini mwa Iran yafikia 40, wengine zaidi ya 1,000 kujeruhiwa
Moshi ukifuka baada ya mlipuko mkubwa kwenye Bandari ya Shahid Rajaee katika Mji wa Bandar Abbas wa Jimbo la Hormozgan, Iran, Aprili 26, 2025. (Shirika la Habari la Mehr/kupitia Xinhua)
TEHRAN - Idadi ya vifo kutoka mlipuko mkubwa kwenye bandari katika jimbo la Hormozgan kusini mwa Iran juzi Jumamosi imefikia 40, na serikali ya nchi hiyo imetangaza siku moja ya maombolezo ya kitaifa, shirika la habari la Iran IRIB limeripoti jana Jumapili.
Mlipuko huo na moto uliofuatia vimeacha watu zaidi ya 1,000 wakiwa wamejeruhiwa, miongoni mwao 197 wamelazwa hospitalini, IRIB limeripoti likimnukuu Gavana wa Hormozgan Mohammad Ashuri Taziani akisema.
Imeelezwa kuwa chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana.
Msemaji wa serikali ya Iran, Fatemeh Mohajerani, katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X, amesema serikali ya nchi hiyo imeitangaza leo Jumatatu kuwa siku ya maombolezo ya kitaifa.
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian alifanya ziara kwenye bandari hiyo jana Jumapili ili kutathmini mazingira ya mlipuko huo, na kutembelea baadhi ya majeruhi, kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi yake.
Hossein Sajedinia, mkuu wa Shirika la Taifa la Usimamizi wa Majanga la Iran, ameliambia IRIB kwamba timu za zima moto kutoka majimbo matano ya nchi hiyo zilikuwa zikifanya kazi kuzuia moto huo, akitabiri kuwa moto huo utadhibitiwa baada ya saa machache.
Amesema baadhi ya makontena yaliyokuwa bandarini hapo yalikuwa na vitu vinavyoweza kushika moto, mfano bereu, na mengine yalikuwa na kemikali ndani yake.
Licha ya tukio hilo, magati ya bandari hiyo yamerejea kufanya kazi na kupakia na kupakua mizigo, kwa mujibu wa shirika la habari la Iran, IRNA.
Moshi ukifuka baada ya mlipuko mkubwa kwenye Bandari ya Shahid Rajaee katika Mji wa Bandar Abbas wa Jimbo la Hormozgan, Iran, Aprili 26, 2025. (Shirika la Habari la Mehr/kupitia Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma