

Lugha Nyingine
Waonyeshaji bidhaa kwenye maonyesho ya biashara ya Zimbabwe wana nia ya kupanua ushirikiano na China
Rachael Dube, meneja mauzo kutoka Samtric Supplies, kampuni ya vifaa vya uchimbaji madini ya Afrika Kusini, akionyesha bidhaa zake kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Zimbabwe mjini Bulawayo, Zimbabwe, Aprili 25, 2025. (Xinhua/Xu Zheng)
BULAWAYO, Zimbabwe – Waonyeshaji bidhaa mbalimbali wa Afrika katika Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Zimbabwe (ZITF) mwaka huu wameonyesha nia yao kubwa ya kupanua ushirikiano wa kibiashara na China, nchi ya pili kwa uchumi mkubwa duniani.
ZITF, maonyesho maarufu ya biashara ya mwaka ya Zimbabwe, yamevutia waonyeshaji zaidi ya 600, wakiwemo washiriki wa kigeni kutoka nchi 28, wakionyesha bidhaa na huduma zao katika maonyesho hayo ya siku sita, yaliyohitimishwa juzi Jumamosi.
Mary Mwalwanda Msukwa, mkurugenzi mtendaji wa Tilawe Products, kampuni ya Malawi inayosambaza mazao ya kilimo, ameelezea matumaini yake ya kutambulisha na kuuza nje nchini China mchele wa Kilombero, mchele mweupe mrefu, wenye harufu nzuri unaolimwa zaidi Malawi.
"Mchele wa Kilombero ni mzuri sana, una ladha nzuri, wenye kunukia vizuri, kwa hiyo tunataka kupenya soko la China, kwa sababu tunajua kwamba tunaweza kupata masoko mengi nchini China," ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua Ijumaa.
Ili kunadi aina hiyo nchini China, Msukwa amepanga kuonyesha mchele huo wa Kilombero na bidhaa nyinginezo kwenye Maonyesho ya Kiuchumi na Biashara ya China na Afrika nchini China, akitarajia kutumia fursa hiyo kuendeleza zaidi uhusiano wa kibiashara na kampuni za China.
Rachael Dube, meneja mauzo kutoka Samtric Supplies, kampuni ya usambazaji vifaa vya uchimbaji madini ya Afrika Kusini, ameonyesha nia kama hiyo ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kampuni za China.
Amesema kuwa kampuni yake tayari ina uzoefu wa kushirikiana na kampuni za uchimbaji madini za China na sasa ina nia ya kupanua ushirikiano huo.
"Kwa vile Zimbabwe na China zimeimarisha ushirikiano wao katika uchimbaji madini, pia inawaletea wasambazaji vifaa kama sisi fursa zaidi, na ndiyo maana tuko hapa kwenye maonyesho ya biashara tukitafuta wateja wengi zaidi na zaidi," amesema.
Malebo Matlala, meneja mwingine wa mauzo kutoka kampuni ya nguo ya Afrika Kusini, ameeleza kwamba kampuni yake imekuwa ikiagiza vitambaa kutoka China ili kuzalisha bidhaa zinazohusiana na utalii.
Huku kukiwa na kuongezeka kwa idadi ya watalii wa China wanaotembelea Afrika kwa safari za utalii, anaona hii kama fursa ya kutangaza bidhaa za kampuni hiyo, kuanzia viatu vya safari hadi mabegi.
"Pia tunajaribu kutafuta kampuni moja ya China ambayo inaweza kutusaidia kutengeneza bidhaa nchini China na kuingia katika soko la China," amesema.
Malebo Matlala, meneja mauzo kutoka kampuni ya nguo ya Afrika Kusini, akionyesha bidhaa zake kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Zimbabwe mjini Bulawayo, Zimbabwe, Aprili 25, 2025. (Xinhua/Xu Zheng)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma