China yaahidi kuchukua hatua zaidi za kuhimiza ajira na uchumi huku kukiwa na hali ya kutokuwa na uhakika duniani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 29, 2025

BEIJING – Katika kukabiliana na hali inayozidi kuongezeka ya kutokuwa na uhakika duniani, China inapanga kutangaza hatua zaidi za kuimarisha kasi ya ukuaji katika kipindi kilichobakia cha mwaka huu, ikilenga kudumisha hali tulivu ya ajira na kufikia malengo ya maendeleo ya mwaka 2025.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jana Jumatatu, maafisa kadhaa waandamizi wa China wamefahamisha juu ya sera zilizopangwa kuhusu kuhimiza zaidi matumizi na kuimarisha mwelekeo wa kufufuka kwa sekta ya nyumba.

Zhao Chenxin, naibu mkuu wa Kamati ya Taifa ya Maendeleo na Mageuzi ya China, ameelezea kwa kina hatua hizo mpya katika maeneo matano muhimu: kuunga mkono ajira, kutuliza biashara ya nje, kuhimiza matumizi, kupanua uwekezaji fanisi, na kujenga mazingira mazuri kwa ajili ya maendeleo.

"Serikali itahimiza biashara kudumisha viwango tulivu vya wafanyakazi na kuanzisha sera zinazosaidia kampuni za kuuza bidhaa nje kupunguza hatari. Hatua zitatangazwa ili kuongeza matumizi ya huduma, kuchochea mauzo ya magari, kuharakisha uwekezaji binafsi, kuanzisha zana mpya za kifedha zenye msingi wa kisera, kuweka soko la mitaji katika hali ya utulivu na uhai, na kuimarisha maendeleo ya soko la nyumba." Zhao amesema.

Akizungumza kwenye mkutano huo na waandishi wa habari, Zou Lan, naibu mkuu wa Benki Kuu ya China, amesema China itapunguza viwango vya mahitaji ya akiba na viwango vya riba kwa wakati mwafaka na kuunda zana mpya za kimuundo za sera ya fedha, kuhakikisha ukwasi wa kutosha ili kujenga utulivu wa ajira na uhimilivu wa uchumi.

"Benki kuu inafuatilia njia za kupanua zana zake za sera, na kupanga kutoa hatua ili kuimarisha misingi ya maendeleo ya uchumi na utulivu wa kijamii," Zou amesema.

Kauli hizo za maafisa hao waandamizi zimekuja huku kukiwa na juhudi zinazoendelea za nchi hiyo kuendana na kukabiliana na changamoto kubwa za kiuchumi duniani huku ikidumisha mwelekeo tulivu wa ukuaji.

Pamoja na ongezeko la kutia moyo la asilimia 5.4 la Pato la Taifa katika robo ya kwanza, watunga sera wa China wametambua mwelekeo mzuri katika mkutano wa ngazi ya juu uliofanyika Ijumaa iliyopita, huku wakionya kwamba kuimarika kwa uchumi kunahitaji kudumishwa zaidi ili kuzuia athari zinazoongezeka kutoka mishtuko ya nje.

Mkutano wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China umetoa wito wa kujiandaa kwa mazingira ya hali mbaya zaidi kwa mipango ya kutosha, na kushughulikia hali ya kutokuwa na uhakika ya mabadiliko makubwa ya mazingira ya nje kwa uhakika wa maendeleo bora ya kiwango cha juu ya nchi hiyo.

Wakati akijibu swali la vyombo vya habari kuhusu "ushuru wa Reciprocal" uliowekwa na Marekani, Zhao ameziita hatua hizo za kujihami kuwa kitendo cha wazi cha ukandamizaji wa upande mmoja, ambacho kinapingana vikali na mielekeo ya kihistoria na sheria za kiuchumi na hakika kitashindwa.

"China itasimama pamoja na nchi nyingi duniani -- katika upande sahihi wa historia na upande wa upigaji hatua wa binadamu," amesema.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha