

Lugha Nyingine
China yaanzisha sera ungaji mkono kurahisisha usafiri na ununuzi kwa watalii wa kimataifa
Watalii kutoka Ufaransa wakitembelea Bustani Yuyuan mjini Shanghai, Mashariki mwa China, Februari 1, 2025. (Xinhua/Chen Haoming)
Kwa Stephanie, mtalii kutoka Australia, safari yake ya kwanza kwenda Shanghai iligeuka kuwa siyo tu uhondo kwa macho bali pia mafanikio kwa mabegi yake ya manunuzi.
"Nimefurahia mandhari na manunuzi hapa," amesema, akiongeza kuwa amechagua vitu vya ukumbusho na nguo, hasa chapa za China ambazo zinazidi kuwa maarufu miongoni mwa Waaustralia.
Kilichomshangaza zaidi ni sera ya China ya marejesho ya kodi wakati wa watalii kuondoka, ambayo imefanya ununuzi uvutie zaidi. "Sera ya marejesho ya kodi wakati wa kuondoka ni kitu kipya kabisa kwangu, na inasaidia sana," amesema.
Stephanie ni miongoni mwa idadi inayoongezeka ya waalii wa kimataifa wanaonufaika na juhudi za China za kurahisisha taratibu za marejesho ya kodi wakati wa kuondoka na kuboresha mazingira ya ununuzi. Siku ya Jumapili, China ilianzisha hatua mpya zinazolenga kuimarisha zaidi sera hiyo ya marejesho ya kodi wakati wa kuondoka na kuchochea matumizi ya wasafiri wanaoingia ndani ya China.
Hatua hizo, zilizotangazwa na Wizara ya Biashara ya China na idara nyingine tano za serikali, zinajumuisha kupunguza kikomo cha chini cha malipo yanayostahili marejesho ya kodi, kuongeza kikomo cha juu cha fedha taslimu zinazorejeshwa, kuongeza mtandao wa maduka yanayoshiriki, na kupanua wigo wa bidhaa zinazopatikana.
Mtalii akitembea kutoka nje ya duka linalorejesha kodi la mzalishaji wa saa ya mkono SEA-GULL mjini Tianjin, Kaskazini mwa China, Desemba 31, 2025. (Xinhua/Yue Yuewei)
Chini ya sera hiyo mpya, kikomo cha kiwango cha chini cha matumizi yanayostahili marejesho ya kodi kimepunguzwa hadi Yuan 200 (takriban dola za Marekani 27.8) kutoka Yuan 500. Marekebisho hayo pia yatawezesha maduka mengi zaidi ya bidhaa maalum, maduka ya vitu vya ukumbusho na zawadi yenye thamani za miamala ya wastani wa chini kujiunga na mpango huo wa marejesho ya kodi.
Serikali ya China pia inapanua idadi ya maduka ya marejesho ya kodi kwa abiria wanaoondoka, huku ikiwa na mipango ya kuongeza sehemu zaidi katika maeneo makuu ya manunuzi, vivutio vya watalii, viwanja vya ndege, hoteli na maeneo mengine muhimu. Maduka hayo yanahimizwa kupanua aina ya bidhaa zinazouzwa, ili kujumuisha chapa zinazothaminiwa kwa muda mrefu, bidhaa maarufu za China, vifaa vya kiteknolojia vya kisasa, vitu vya urithi wa utamaduni usioshikika, kazi za sanaa za mikono na bidhaa maalum, miongoni mwa nyinginezo.
China pia inakuza mfumo wa "marejesho ya kodi wakati wa ununuzi", ukiruhusu watalii wanaostahili kupokea marejesho ya kodi papo hapo kwenye maduka ya kuuza reja reja badala ya kusubiri hadi waondoke China. Ukomo wa marejesho ya fedha taslimu umeongezwa mara mbili kutoka Yuan 10,000 hadi Yuan 20,000.
China ilianzisha sera ya marejesho ya kodi kwa watalii wanaoondoka nje ya nchi mwaka 2015. Kwa mujibu wa takwimu za serikali, mwaka jana, mauzo ya bidhaa zinazostahili marejesho ya kodi yaliongeza kwa asilimia 120 ikilinganishwa na mwaka uliopita, wakati huohuo jumla ya kiasi cha kodi kilichorejeshwa iliongezeka kwa asilimia 130. Watalii wanaoingia China walitumia jumla ya dola za Marekani bilioni 94.2 mwaka jana, ongezeko la asilimia 77.8 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma