Dunia inahitaji Ushirikiano, Si Mgawanyiko | Maoni People's Daily Online kuhusu Utozaji Kiholela wa Kodi wa Marekani 2

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 30, 2025

Maendeleo si haki ya kipekee ya Marekani, bali ni haki ya wote kwa nchi zote duniani. Nchi zilizoendelea zina wajibu wa kusaidia nchi zinazoendelea kuboresha uwezo wao wa maendeleo, badala ya kutumia nguvu zao kuzuia mchakato wa maendeleo wa nchi zingine.

Katika muktadha wa kuongezeka kufungamana kwa karibu kwa uchumi wa dunia, utozaji kiholela wa ushuru wa Marekani ni sawa na kuzinyima nchi, hasa zile za Dunia ya Kusini haki ya maendeleo.

"Tunahitaji ushirikiano, si mgawanyiko", ni sauti ya pamoja ya nchi kote duniani. Katika siku za hivi karibuni, nchi zaidi zimetoa sauti kali zaidi juu ya kile kinachoitwa sera ya “ushuru wa kutozana kwa usawa” ya Marekani. Serikali nyingi, zikiwemo za Ufaransa, Uingereza, Italia, Australia, zimeeleza upinzani wao. Peru, Kazakhstan na Chad na nchi zingine zimelaani vikali sera hiyo ya Marekani kwa kuleta madhara makubwa kwa nchi zinazoendelea zenye uchumi dhaifu.

Kipekee, baadhi ya viongozi wa nchi mbalimbali pia wamezungumzia suala hilo. Waziri Mkuu wa Singapore, Lawrence Wong, ameikosoa Marekani kwa kukiuka makubaliano ya biashara huria; Waziri Mkuu wa Malaysia, Anwar Ibrahim, ametoa wito kwa nchi za ASEAN kushikamana na kukabiliana na sera hiyo ya ushuru ya Marekani.

Aprili 23, China iliitisha mkutano wa Baraza la Usalama kwa muundo wa Arria kuhusu “Athari za Hatua za Upande Mmoja na Ubabe kwa Uhusiano wa Kimataifa”. Wawakilishi kutoka nchi zaidi ya 80, zikiwemo nchi wanachama wa Baraza hilo, walihudhuria. China ilipaza sauti yake ya haki dhidi ya ubabe wa upande mmoja, na sehemu kubwa ya nchi zilizoshiriki zimetoa wito wa kushikilia mfumo wa pande nyingi na kuimarisha mazungumzo na ushirikiano.

Dunia haiwezi kulipia gharama ya msukosuko wa Marekani. Dunia ya leo inalazimika kusonga mbele kuelekea muundo wa kimataifa ulio wa haki na usawa zaidi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha