Umoja wa Mataifa watafuta msaada wa dharura kwa waathirika 45,000 wa mafuriko nchini Somalia

(CRI Online) Mei 02, 2025

Ofisi ya Kuratibu misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA), imetoa wito wa msaada wa dharura wa haraka kusaidia watu 45,000 walioathiriwa na mafuriko kote nchini Somalia.

OCHA imesema watu wanne, wakiwemo watoto wawili, wamepoteza maisha baada ya kusombwa na maji, huku zaidi ya watu 45,000 wakiwa wameathiriwa na mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua za wastani hadi kubwa katika majimbo mbalimbali ya Somalia tangu Aprili 15.

Jumatatu wiki hii Mto Shabelle ulipasua kingo katika wilaya ya Jowhar, na kufanya zaidi ya watu 6,000 kuhama makazi yao na takriban hekta 11,000 za ardhi kuharibwa.

OCHA imetoa wito wa msaada hasa kuhusu makazi, vituo vya usafi, na msaada wa kuhamisha watu.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha