

Lugha Nyingine
Vikosi vya wanamgambo wa Sudan vyazidisha mashambulizi ya droni kwenye maeneo yanayodhibitiwa na jeshi
Moshi na moto vikionekana baada ya shambulizi la droni kwenye ghala la mafuta mjini Port Sudan, mashariki mwa Sudan, Mei 5, 2025. (Wizara ya Nishati na Petroli ya Sudani/kupitia Xinhua)
KHARTOUM – Wanamgambo wa Sudan wa Vikosi vya Mwitikio wa Haraka (RSF) hivi karibuni wamekuwa wakizidisha mashambulizi ya droni kwenye maeneo yanayodhibitiwa na Jeshi la Sudan, hatua mpya ambayo wataalamu wa kijeshi wanaichukulia kuwa ni kuongezeka kwa hatari katika mgogoro huo unaoendelea kati yao.
Kwa siku ya pili mfululizo, kundi la droni, zinazodaiwa kurushwa na RSF, zimekuwa zikilenga vituo muhimu mjini Port Sudan, mji mkuu wa Jimbo la Bahari Nyekundu la mashariki. Tangu Mei 2023, mji huo wa bandari umekuwa ukitumika kama mji mkuu wa muda wa nchi hiyo, makao ya serikali na jumbe za kidiplomasia.
"Droni zimepiga maghala ya mafuta ya mji mapema asubuhi, na kusababisha milipuko mikubwa, moto, na moshi mwingi," shuhuda mmoja ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.
Video zilizowekwa mitandaoni na wanaharakati zinaonyesha timu za ulinzi wa raia zikijaribu kuudhibiti moto huo na kuuzuia usisambae kwenye mabohari mengine. Hakuna vifo vya watu vilivyoripotiwa hadi kufikia sasa.
Wakati akitembelea eneo lililolengwa, Waziri wa Nishati wa Sudan, Mohieddin Naeem Mohamed Saeed ameshutumu shambulizi hilo kuwa ni "kitendo cha kigaidi" kilichokusudiwa kuharibu maghala makubwa zaidi ya mafuta katika Jimbo la Bahari Nyekundu.
Waziri huyo ameyaelezea mashambulizi hayo kuwa ya mpya zaidi katika mfululizo wa mashambulizi yaliyoratibiwa ya wanamgambo hao dhidi ya huduma za umma na miundombinu ya kiraia, yakiathiri moja kwa moja maisha ya raia.
Matukio hayo yametokea siku moja baada ya droni za RSF kulenga kambi ya jeshi la anga, ghala la mizigo na miundombinu ya kiraia mjini Port Sudan, likiwa ni shambulizi la kwanza katika mji huo tangu mgogoro huo kuzuka katikati ya Aprili 2023.
Pia siku hiyo ya Jumatatu, chanzo cha habari cha kijeshi kimeliambia Xinhua kwamba mifumo ya ulinzi wa anga wa jeshi umezuia kundi la droni zilizolenga Uwanja wa Ndege wa Kassala, mji mkuu wa Jimbo la Kassala mashariki mwa Sudan. Mji huo umekuwa ukikumbwa na mashambulizi ya droni kwa siku ya tatu mfululizo, kwa mujibu wa chanzo hicho.
Chanzo hicho, kikizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, kimesema kuwa majira ya saa 11 alfajiri kwa saa za huko (0300 GMT), droni nne zilijaribu kupiga Uwanja wa Ndege wa Kassala lakini zilizuiliwa kwa mafanikio na mifumo ya ulinzi ya ardhini, na hakuna hasara iliyoripotiwa.
Gavana wa Jimbo la Kassala, Al-Sadiq Mohamed Al-Azraq, amewaambia waandishi wa habari siku hiyo ya Jumatatu kwamba "mji wa Kassala unakabiliwa na vitisho vinavyoongezeka kutoka kwa droni," akitoa wito kwa uongozi wa kitaifa kuingilia kati na kuhakikisha usalama wa uwanja wa ndege.
Wakati huo huo, vyombo vya habari vya nchini humo vimeripoti shambulizi jipya la droni kwenye Bwawa la Merowe kaskazini mwa Sudan baadaye Jumapili, ingawa hakuna uthibitisho rasmi ambao umetolewa.
Tangu Jeshi la Sudan lilipodhibiti tena maeneo mengi ya mji mkuu, Khartoum, mwezi Machi, RSF imekuwa ikiongeza mashambulizi ya droni katika maeneo yanayoshikiliwa na jeshi hilo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma