TBS yateketeza tani 43 za vipodozi visivyokidhi viwango na nguo za ndani za mitumba kutoka nje ya nchi

(CRI Online) Mei 06, 2025

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeteketeza tani 43 za vipodozi visivyokidhi viwango na nguo za ndani za mitumba zilizoingizwa nchini humo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Candida Shirima alisema Jumatatu kuwa vipodozi na nguo za ndani za mitumba zilizoteketezwa zilikamatwa kati ya Julai 2024 na Februari 2025.

Shirima, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ufuataji na Usimamizi wa Utekelezaji Sheria wa TBS, amesema vipodozi na nguo za ndani zisizokidhi viwango vilikamatwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

Shirima ametoa wito kwa wananchi kuacha kununua vipodozi visivyokidhi viwango na nguo za mitumba kutoka nje kwa sababu za kiafya.

Pia amehimiza waagizaji vipodozi na nguo za mitumba kuhakikisha bidhaa zao zinakidhi viwango vinavyotakiwa ili kuepusha hasara inayotokana na uteketezaji wa bidhaa zisizokidhi viwango.

Shirima ameongeza kuwa TBS itaendelea kukagua mara kwa mara bidhaa zinazotoka nje ya nchi ili kuhakikisha zinakidhi viwango vinavyotakiwa.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha