AU na IGAD zasisitiza tena "uungaji mkono usioyumba" kwa ajili ya utulivu na maendeleo ya Sudan Kusini

(CRI Online) Mei 07, 2025

Umoja wa Afrika (AU) na Mamlaka ya Kiserikali kwa Maendeleo ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD), wamesisitiza tena "uungaji mkono wao usioyumba" kwa ajili ya amani na maendeleo endelevu nchini Sudan Kusini.

Haya yanajiri wakati Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Mahmoud Ali Youssouf alipofanya ziara rasmi ya siku mbili mjini Juba, Sudan Kusini, Jumatatu na Jumanne, kwa uratibu wa karibu na IGAD.

Ziara hiyo ya ngazi ya juu ililenga kushirikiana na mamlaka ya Sudan Kusini na wadau wakuu kuhusu hali inayoendelea ya kisiasa na usalama, vilevile hali ya mchakato wa amani nchini humo.

Mashirika hayo mawili yamesisitiza kuwa amani, utulivu na utawala jumuishi ni "misingi muhimu" kwa maendeleo endelevu ya Sudan Kusini na ushirikiano wa kikanda.

Yametilia mkazo hitaji la dharura la kuzidisha kuaminiana, mshikamano wa kitaifa, heshima kwa nafasi ya kisiasa na ya kiraia, na kuendelea na dhamira ya mazungumzo na maelewano kati ya wadau wa kisiasa wa Sudan Kusini.

Wakati wa ziara yake, mwenyekiti wa Kamisheni ya AU alifanya mashauriano ya ngazi ya juu na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na maafisa wengine waandamizi wa serikali.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha