China yatangaza uungaji mkono mpya wa sera kuchochea ufufukaji wa uchumi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 08, 2025

Ofisi ya Habari ya Baraza la Serikali la China ikifanya mkutano na waandishi wa habari juu ya sera za mambo ya fedha ili kutuliza soko na matarajio, mjini Beijing, mji mkuu wa China, Mei 7, 2025. (Xinhua/Li He)

Ofisi ya Habari ya Baraza la Serikali la China ikifanya mkutano na waandishi wa habari juu ya sera za mambo ya fedha ili kutuliza soko na matarajio, mjini Beijing, mji mkuu wa China, Mei 7, 2025. (Xinhua/Li He)

BEIJING - Mamlaka za fedha na mambo ya kifedha za China zimetangaza hatua mbalimbali za ungaji mkono jana Jumatano, zikiwemo kupunguza viwango vya sera na uwiano wa mahitaji ya akiba (RRR), wakati ambapo nchi hiyo inaongeza juhudi za kutuliza masoko na kuendeleza ufufukaji wa uchumi huku kukiwa na changamoto za nje.

Katika moja ya hatua zake kuu za kisera, Benki Kuu ya China (PBOC), imetangaza punguzo la RRR la asilimia 0.5 kwa taasisi stahiki za fedha kuanzia Mei 15. Haswa, RRR kwa ajili ya ufadhili wa magari na kampuni za kuazima fedha itapunguzwa kutoka asilimia 5 hadi 0.

Mkuu wa benki kuu ya China Pan Gongsheng amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari kwamba hatua hiyo inatarajiwa kulipatia soko la fedha yuan takriban trilioni 1 (dola za Kimarekani kama bilioni 138.9) katika ukwasi wa muda mrefu.

Benki kuu ya China Jumatano pia imetangaza uamuzi wake wa kupunguza kiwango cha Reverse REPO kwa siku saba kwa asilimia 0.1 kuanzia Alhamisi ili kutekeleza vyema sera ya fedha iliyolegea kiasi na kuimarisha uungaji mkono kwa uchumi halisi.

Pan amesema upunguzaji huu wa kiwango cha sera unatarajiwa kusababisha kiwango cha msingi cha mkopo (LPR), kiwango cha ukopeshaji chenye msingi wa soko, kushuka kwa asilimia 0.1.

Wakati huo huo, ungaji mkono zaidi wa kifedha utatolewa kwa sekta zikiwemo za uvumbuzi wa teknolojia, matumizi ya huduma na huduma kwa wazee kupitia utoaji mikopo kwa mara ya pili -- huku viwango vya kukopesha tena vikipungua kwa asilimia 0.25 kuanzia jana Jumatano, benki kuu hiyo imesema.

Kuimarika kwa soko la mitaji

Pia akizungumza na waandishi wa habari, Wu Qing, Mkuu wa Kamisheni ya Udhibiti wa Dhamana ya China (CSRC), ameahidi juhudi za kuweka soko la mitaji kuwa tulivu na hai, akisema kuwa kamisheni hiyo itasaidia kampuni zilizoathiriwa na ushuru kukabiliana vizuri na changamoto.

"Mamlaka husika zitaunga mkono kampuni katika kutumia zana mbalimbali za kifedha kama vile hisa, dhamana na amana za uwekezaji wa nyumba (REITs) kukusanya mitaji moja kwa moja, na kuhimiza kampuni stahiki za ndani kuingia kwenye masoko ya hisa ya nchi za nje kwa kufuata sheria na kanuni," Wu ameviambia vyombo vya habari.

Uimarishaji soko la nyumba

Mamlaka za China pia zitaharakisha uanzishaji wa mfululizo wa mifumo ya kukusanya mitaji inayowiana na mtindo mpya wa maendeleo wa sekta ya nyumba, na kuimarisha juhudi za kutuliza soko la nyumba, Li Yunze, Mkuu wa Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi na Ukaguzi wa Mambo ya Fedha ya China amesema kwenye mkutano huo na waandishi wa habari.

“Mikopo iliyoidhinishwa kwa ajili ya miradi ya nyumba kwenye "orodha nyeupe" ya China imefikia yuan trilioni 6.7, ambayo imewezesha ujenzi na ukamilishaji wa nyumba zaidi ya milioni 16, na kwa kiasi kikubwa kuzuia kudorora kwa sekta ya nyumba na kurejesha utulivu wa soko,” Li amesema.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha