Kamanda mkuu wa jeshi la Iran ahoji ahadi ya Israel ya kusimamisha vita

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 30, 2025

Mazishi ya kiserikali ya makamanda wa kijeshi na wanasayansi wa nyuklia waliouawa na Israeli wakati wa vita vya siku 12 yakifanyika Tehran, Iran, Juni 28, 2025. (Xinhua)

Mazishi ya kiserikali ya makamanda wa kijeshi na wanasayansi wa nyuklia waliouawa na Israeli wakati wa vita vya siku 12 yakifanyika Tehran, Iran, Juni 28, 2025. (Xinhua)

TEHRAN - Abdolrahim Mousavi, mkuu wa Jeshi la Iran amehoji ahadi ya Israel kwa makubaliano ya hivi karibuni ya kusimamisha vita kufuatia siku 12 za mapigano, akionya kwamba Tehran imejiandaa kujibu kwa nguvu uchokozi wowote utakaofanywa upya, kwa mujibu wa shirika la habari la Iran, Tasnim.

Mousavi, ametoa kauli hiyo jana Jumapili alipozungumza kwa njia ya simu na Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia Prince Khalid bin Salman, wakati wawili hao wakijadili mgogoro unaohusisha Iran, Israel na Marekani.

"Tuna mashaka makubwa juu ya ufuataji makubaliano ya kusimamisha vita wa adui," Mousavi amesema, akiongeza: "Kama uchokozi unarudiwa, tuko tayari kujibu kikamilifu."

Amezishutumu Israel na Marekani kwa kuanzisha mashambulizi dhidi ya Iran licha ya kile alichokieleza kuwa ni kujizuia kwa Tehran, ikiwemo wakati wa mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja na Marekani.

Kwa upande wake, waziri wa ulinzi wa Saudi Arabia amelaani "uchokozi" dhidi ya Iran na kusema Riyadh imefanya juhudi za kusaidia kumaliza mgogoro huo, shirika hilo la habari la Tasn limeripoti.

Pande hizo mbili pia zimekubaliana kudumisha mashauriano yenye lengo la kuboresha uhusiano kati ya pande mbili na kuhimiza utulivu wa kikanda.

Kwa wakati tofauti, naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa, Majid Takht-Ravanchi, amesema Tehran haijapanga mkutano wowote na maafisa wa Marekani, akikanusha madai ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani ya mazungumzo yajayo ya nyuklia, vyombo vya habari vya serikali vimeripoti.

Akizungumza mwishoni mwa mkutano wa kilele wa NATO mapema wiki iliyopita, Rais Trump alisema maafisa wa Marekani na Iran watakuwa wakikutana wiki inayofuata (wiki hii) kujadili makubaliano ya nyuklia yanayowezekana kufikiwa.

Mgogoro huo ulipamba moto Juni 13 wakati Israel ilipofanya mashambulizi ya anga katika ardhi ya Iran, yakilenga vituo vya kijeshi na nyuklia. Mashambulizi hayo yameua makamanda waandamizi, wanasayansi wa nyuklia na raia, kwa mujibu wa maafisa wa Iran.

Iran ililipiza kisasi kwa mawimbi ya mashambulizi ya makombora na droni dhidi ya Israel. Juni 22, vikosi vya Marekani vilishambulia kwa mabomu vituo vitatu vya nyuklia vya Iran - Fordow, Natanz, na Isfahan. Katika kujibu, Iran ilipiga kambi za kikosi cha anga cha Marekani ya Al Udeid nchini Qatar.

Usimamishaji huo vita kati ya Iran na Israel ulifikiwa Jumanne wiki iliyopita baada ya wiki takriban mbili za mapigano.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha