Huawei yafanya maonesho ya ajira kwa wahitimu wa TEHAMA nchini Uganda

(CRI Online) Julai 03, 2025

Kampuni ya teknolojia ya China Huawei imezindua maonesho ya mwaka ya ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu nchini Uganda jana Jumatano, ikilenga kuunganisha wahitimu na fursa za ajira katika sekta ya Teknolojia ya Upashanaji Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini humo.

Maonesho hayo ya siku moja, yenye kaulimbiu ya "A Better U for a Better Uganda", yalifanyika katika Chuo Kikuu cha Kyambogo mjini Kampala, yakivutia mamia ya wanafunzi na wahitimu wa TEHAMA.

Mkurugenzi wa mambo ya kidijitali wa kampuni hiyo ya Huawei tawi la Uganda Bw. Julius Mugume, amesema maonesho hayo yanatoa mfumo wa mafunzo ya jumla kwa waajiriwa wapya kwa ajili ya maendeleo yao katika ajira.

Msemaji wa Huawei Uganda, Sooma Mukyala Fouziya amesema, Huawei inalenga kuunga mkono ukuaji wa jumuiya ya teknolojia ya Uganda kupitia kuwapatia wataalam vijana nyenzo, rasilimali na majukwaa wanayohitaji kustawi katika sekta ya TEHAMA inayokua kwa kasi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha