

Lugha Nyingine
China na DPRK zasisitiza tena urafiki, zaahidi uhusiano wa karibu wakati viongozi wakuu wakifanya mazungumzo
Xi Jinping, Rais wa China ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akifanya mazungumzo na Kim Jong Un, Katibu Mkuu wa Chama cha Labor cha Jamhuri ya Kidemokrasi ya Watu ya Korea (DPRK), ambaye pia ni mwenyekiti wa mambo ya kitaifa wa nchi hiyo kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing Septemba 4, 2025. (Xinhua/Huang Jingwen)
BEIJING - Viongozi wakuu wa China na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu ya Korea (DPRK) wamesisitiza tena urafiki wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili jirani, wakiahidi kuendeleza zaidi uhusiano wa pande mbili.
Habari hizo zimetolewa wakati Xi Jinping, Rais wa China ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), alipofanya mazungumzo na Kim Jong Un, Katibu Mkuu wa Chama cha Labor cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu ya Korea, ambaye pia ni mwenyekiti wa mambo ya kitaifa wa nchi hiyo mjini Beijing.
Rais Kim Jong Un alikuja China kuhudhuria maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 80 tangu kupatikana ushindi katika Vita vya Watu wa China vya Kupambana na Uvamizi wa Japan na Vita vya Dunia vya Kupinga Ufashisti.
Rais Xi amesema, "Hii imeonesha dhamira kubwa ya DPRK ya kulinda matokeo ya ushindi katika Vita vya Pili vya Dunia, na kutoa fursa muhimu kwa vyama viwili na nchi hizo mbili kuendeleza uhusiano wa urafiki na ushirikiano," akiongeza kuwa China na DPRK ni majirani wema, marafiki wazuri na makomredi wema wenye nia sawa, Imani na matarajio ya pamoja na kuungana mkono.
"Chama cha CPC na serikali ya China vinathamini sana urafiki wa jadi kati ya nchi hizo mbili na vinapenda kudumisha, kuimarisha na kuendeleza uhusiano mzuri kati ya China na DPRK," Rais Xi amesema.
Amesema kuwa, China inapenda kuimarisha mawasiliano kwenye ngazi ya juu na uratibu wa kimkakati, kubadilishana mawazo kwa kina kuhusu uzoefu katika utawala wa chama na nchi , na kuongeza maelewano na urafiki kati ya China na DPRK.
Kuhusu suala la Peninsula ya Korea, Rais Xi amesema China siku zote inafuata msimamo wa kufuata hali halisi na haki, na kutopendelea upande wowote, na inapenda kuendelea kuimarisha uratibu na DPRK na kufanya juhudi za kudumisha amani na utulivu wa peninsula hiyo.
Rais Kim, kwa upande wake, amesema kuwa viongozi wa vizazi vikongwe wa DPRK na China, wakati wa vita vya mapambano dhidi ya uvamizi wa Japan, walianzisha kiunganishi cha uhusiano mkubwa, ambao nchi hizo mbili zinabeba wajibu wa kuurithisha kizazi hadi kizazi.
"Haijalishi jinsi gani hali ya kimataifa inavyobadilika, urafiki kati ya DPRK na China utabaki bila kubadilika, na ni dhamira thabiti ya DPRK kuimarisha na kuendeleza siku hadi siku uhusiano wa pande mbili," ameongeza.
Xi Jinping, Rais wa China ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akifanya mazungumzo na Kim Jong Un, Katibu Mkuu wa Chama cha Labor cha DPRK , ambaye pia ni mwenyekiti wa mambo ya kitaifa wa nchi hiyo, katika Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing Septemba 4, 2025. (Xinhua/Ding Lin)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma