Lugha Nyingine
Wanamgambo wa Houthi wa Yemen wadai kuhusika na mashambulizi ya droni dhidi ya Israel

Picha hii ya kumbukumbu ikionyesha Uwanja wa Ndege wa Ramon karibu na mji wa pwani ya Bahari Nyekundu wa Eilat, Israel. (XinhuaJINI)
SANAA - Kundi la wanamgambo la Houthi la Yemen limesema jana Jumapili lilifanya mashambulizi manane ya droni dhidi ya Israeli, likiwemo shambulizi kwenye Uwanja wa Ndege wa Ramon kusini mwa Israel na kuwajeruhi watu kadhaa mapema siku hiyo.
Katika taarifa iliyotolewa na Televisheni ya al-Masirah inayoendeshwa na Wahouthi, msemaji wa jeshi la kundi hilo Yahya Sarea amesema wanamgambo wa Houthi wamerusha "droni nane zikilenga Negev, Eilat, Ashkelon, Ashdodi na Tel Aviv."
Amesema droni moja imepiga Uwanja wa Ndege wa Ramon na kuulazimisha kufungwa na kusimamisha usafiri wa anga, huku droni nyingine zikilenga maeneo nyeti ya kijeshi katika miji tofauti.
"Tunathibitisha kuongezeka kwa operesheni zetu za kijeshi na hatutarudi nyuma kutoka kwenye msimamo wetu katika kuunga mkono Gaza," amesema, akionya mashirika ya ndege kuepuka anga na viwanja vya ndege vya Israeli.
Msemaji wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ya Israel amethibitisha mapema siku hiyo kwamba droni ya Houthi ilipiga ukumbi wa watu wanaowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Ramon, kiwanja kidogo kiasi kilicho umbali wa karibu kilomita 18 kaskazini mwa Eilat.
Kikosi cha uokoaji cha Magen David Adom cha Israel kimesema watu takriban wawili wamejeruhiwa kidogo na kupelekewa hadi hospitali moja katika mji wa mapumziko wa karibu wa Eilat. Baadhi ya vyombo vya habari vya Israel vinaweka idadi hiyo ya waliojeruhiwa kuwa wanane.
Wanamgambo hao wa Houthi, ambao wanadhibiti sehemu kubwa ya kaskazini mwa Yemen, wamekuwa wakiilenga Israel tangu Novemba 2023 ili kuonyesha mshikamano na Wapalestina katika ukanda wa Gaza.
Israel imekuwa ikijibu kwa mashambulizi ya kulipiza kisasi ya mara kwa mara, ikiwemo shambulizi la anga mwezi uliopita mjini Sanaa ambalo liliua viongozi 12 wa kundi hilo la Houthi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



