

Lugha Nyingine
China kuwasilisha mahitaji ya msaada wa maafa nchini Afghanistan haraka iwezekanavyo
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China amesema China itafanya kazi na Afghanistan ili kwa pamoja kuvuka wakati mgumu na kuwasilisha mahitaji ya msaada wa maafa katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi haraka iwezekanavyo.
Msemaji Lin Jian ametoa ahadi hiyo kwenye mkutano na wanahabari jana Jumatatu alipoulizwa kuhusu mwitikio wa China baada ya tetemeko la ardhi lililotokea usiku wa manane nchini Afghanistan siku ya Agosti 31.
Lin amesema kuwa China inafuatilia kwa karibu tetemeko hilo la ardhi.
Amesema, Rais Xi Jinping wa China alipokuwa akiongoza Mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) Plus mjini Tianjin, alitoa rambirambi kwa watu waliopoteza maisha katika tetemeko hilo la ardhi na pole kwa wale wote waliopoteza wapendwa wao na watu katika maeneo yaliyoathirika, akiitakia serikali na watu wa Afghanistan kuondokana na wakati huo mgumu na kujenga upya makazi yao.
Amesema, Serikali ya China imetangaza kuipatia Afghanistan msaada wa dharura wa kibinadamu wenye thamani ya Yuan milioni 50 (sawa na dola za Kimarekani milioni 7.04) kwa ajili ya kukabiliana na tetemeko hilo la ardhi, ikiwa ni pamoja na mahema, mablanketi, maturubai, chakula na vifaa vingine vinavyohitajika haraka.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma