Lugha Nyingine
Waziri Mkuu wa Ufaransa Bayrou apoteza kura ya imani juu yake kutokana na kupunguza bajeti

Waziri Mkuu wa Ufaransa Francois Bayrou akitoa taarifa yake ya sera ya jumla kabla ya kura ya imani juu yake kuhusu mpango wa kupunguza bajeti, mjini Paris, Ufaransa, Septemba 8, 2025. (Picha na Aurelien Morissard/Xinhua)
PARIS - Waziri Mkuu wa Ufaransa Francois Bayrou amepoteza kura ya imani naye jana Jumatatu katika Bunge la Taifa la Ufaransa kuhusu mpango wake wa bajeti unaotaka kuokoa mabilioni ya euro kwa mwaka katika matumizi ya serikali ambapo kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Spika wa Bunge la Ufaransa, Yael Braun-Pivet, ni kura 194 pekee ndizo zilizomuunga mkono Bayrou kati ya kura 558 halali.
Hii inamaanisha kuwa mara ya kwanza katika historia ya Jamhuri ya Tano ya Ufaransa kwa serikali kuanguka wakati wa kura ya imani, vyombo vya habari nchini humo vimeripoti.
Awali akizungumza na wabunge Jumatatu alasiri kabla ya upigaji kura, Bayrou alisisitiza kuwa deni kubwa la Ufaransa ni lenye "kuhatarisha uhai" kwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi, deni la umma la Ufaransa lilikuwa limefikia euro bilioni 3,345.8 (dola za kimarekani karibu bilioni 3,914.6), au asilimia 114 ya Pato la Taifa, hadi ilipofikia mwishoni mwa robo ya kwanza ya 2025.
"Ukweli utabaki kuwa usioweza kuzuilika, matumizi yataendelea kuongezeka, na mzigo wa deni, ambao tayari hauwezi kubebeka, utakua mzito na wa gharama kubwa," Bayrou alisema, akihimiza nchi hiyo "kuchukua hatua bila kuchelewa."
"Inahitaji tu uhamasishaji na juhudi za wastani kutoka kwa kila mmoja, mradi tuchukue hatua kwa wakati," alisisitiza.
Katika hotuba yake kabla ya upigaji kura, Marine Le Pen, aliyekuwa mgombea wa kiti cha urais wa chama cha mrengo mkali wa kulia cha Ufaransa, National Rally, alitoa wito kwa Rais Emmanuel Macron kulivunja Bunge ili kuandaa uchaguzi mpya kufuatia kushindwa kwa Bayrou.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Ikulu ya Ufaransa, Elysee imesema kuwa Rais Macron "amekubali" matokeo ya kura hiyo. "Atakutana na Waziri Mkuu Francois Bayrou kesho kukubali kujiuzulu kwa serikali yake," Elysee imesema, ikiongeza kuwa, Rais Macron atamteua waziri mkuu mpya katika siku zijazo.
Msukosuko wa kisiasa nchini Ufaransa umetikisa kote Ulaya. Siku hiyo ya Jumatatu jioni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Antonio Tajani aliviambia vyombo vya habari kwamba "anatumai" suluhu ya mzozo wa kisiasa wa Ufaransa itapatikana "haraka iwezekanavyo," akielezea wasiwasi juu ya athari zake zinazoweza kutokea kwa bara zima.
Rais Macron alimteua Francois Bayrou kuwa waziri mkuu mpya wa Ufaransa Desemba 13, 2024, akichukua nafasi ya Michel Barnier, ambaye aliondolewa katika kura ya kutokuwa na imani naye wiki moja kabla.
Bayrou ni waziri mkuu wa nne wa Ufaransa aliyeteuliwa mwaka 2024 na Rais Macron. Alizaliwa mwaka 1952 na kuanzisha chama cha mrengo wa kati cha Democratic Movement (MoDem) mwaka 2007. Aliwahi kugombea nafasi ya urais mara tatu, mwaka 2002, 2007, na 2012.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



